Tuesday, June 26, 2012

Muendelezo wa kesi ya lulu,Mahakama yaipiga kalenda hadi julai 9, 2012


Msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael (Lulu) akikimbilia basi la Magereza mara baada ya kutoka kusikiliza kesi ya mauaji inayomkabili kwenye Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam.

Maombi ya msanii wa filamu Elizabert Michael ya kuchunguzwa umri wake yameshindwa kusikilizwa leo Mahakama Kuu Kanda ya dare s Salaam na kusogezwa mbele hadi Julai 9, mwaka huu baada ya upande wa mashitaka kuomba maombi yasisikilizwe leo.   Wakili wa serikali Elizabeth Kadanda aliiomba Mahakama hiyo kuahirisha au kusitisha kusikiliza maombi hayo leo kwasababu wamewasilisha maombi mahakama ya Rufaa kupinga uamuzi wa jaji anayesikiliza maombi hayo, Dk Fauz Twaib. 

   Uamuzi uliopingwa ni ule ambao Dk Twaib aliutoa Juni 11 mwaka huu kukubali kusikiliza maombi ya kuchunguza umri wa Lulu ili kujua umri wake halisi baada ya kuwa na utata upande wa mashitaka unadai Lulu ana miaka 18 wakati yeye anadai ana miaka chini ya hiyo.   Baada ya maombi ya wakili Kaganda kuomba maombi yasisikilizwe leo kwa sababu tayari amekatia rufaa uamuzi wa jaji huyo, mawakili wa Lulu, Peter Kibatala na Kennedy Fungamtama walisimama kwa nyakati tofauti na kuwasilisha hoja zao kuwa wanapinga vikali maombi ya Kaganda.   Walidai ni kinyume cha sheria kwa sababu hakukuwa na amri yoyote kutoka mahakama ya rufaa kuzuia usikilizwaji huo hata hivyo upande wa mashitaka ulionyesha kila dalili kuwa maombi leo yatasikilizwa kwa kuwasilisha viapo pamoja na vielelezo vyao kama mahakama ilivyowataka.  

  Walidai pia kuwa maombi hayo inaonyesha yameifikia mahakama ya rufaa asubuhi hiyo ingawa walikiri huwa yamesajiliwa na kupewa namba, walidai kuwa hiyo ni janja ya ofisi ya mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuchelewesha.   Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Dk Twaib alitoa nafasi kwa wakili kaganda kujibu hoja za upande wa utetezi hata hivyo Kaganda hakuwa na majibu ya hapo akaomba nafasi kama yadakika kumi kujiandaa na kufanya mawasiliano na aliporudi hakuwa na hoja zaidi ya kusisitiza maombi yake ya ahirisho kutoa nafasi kwa mahakama ya rufaa kusikiliza maombi yao.  

  Jaji Dk Twaib katika uamuzi wake alikubaliana na maombi ya Kaganda akisema kuwa kwakuwa maombi yameshapokelewa na mahakama ya rufaa na kusajiliwa, wakati wowote zitatakiwa mwenendo mzima wa kesi hivyo hana budi kuahirisha hadi Julai 9 mwaka huu.   Uamuzi huo haukumfurahisha Lulu alilia huku akifuta machozi baada ya kuona kuwa maombi hayo kwa siku hiyo yamegonga mwamba hayatasikilizwa mpaka kusubiri amri ya mahakama ya Rufaa.   Hata hivyo jaji huyo alitoa amri nyingine kuwa haitakiwi mahakama ya Kisutu kuendelea na kesi hiyo mpaka pale uamuzi utakapotoka mahakama hizo za juu, uamuzi ambao ulipuuzwa kama alivyodai wakili Fungamtama kuwa Lulu alipelekwa Kisutu na kesi ilitajwa katika jalada lililofunguliwa la muda.   Katika maombi hayo, tayari upande wa jamuhuri katika maandalizi ya kusikiliza ulikuwa umeshawasilisha Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahohjiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja kuthibitisha kwamba umri wa Lulu ni zaidi ya miaka 18. Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva.



Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.

Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya mawakili wake wanaomtetea kudai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha. Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria ili kulinda maslahi.

Mawakili wa Lulu waliwasilisha viapo vya wazazi wake,

cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa  Dar eS Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.

Viapo  vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995  katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.

Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa,  mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.

Viapo hivyo vinaendelea kueleza kuwa baada ya majadiliano wote, yeye mama, baba na ndugu wengine walikubaliana kuwa wamuite Diana Elizabeth Michael Kimemeta. alibatizwa katika Kanisa la Katoliki  Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta

Utata wa umri wa mshtakiwa huyo uliibuka Mei 7, 2012 katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya wakili wake Fungamtama kudai kuwa ana miaka 17 Mahakama ya Kisutu iliyakataa maombi hayo ikisema kuwa haina mamlaka ya kuyashughulikia na kushauri maombi hayo yawasilishwe Mahamaka Kuu. 

No comments:

Post a Comment