Friday, August 31, 2012

BURIANI BI. HAWA NGURUME

Bi Hawa Ngurume enzi za uhai wake

Aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na Mbalali Mkoani Iringa Bi Hawa Ngurume amefariki dunia.,
Taarifa ilizopata Darbase blog, zimesema mwanamama huyo ambaye enzi za uhai wake alikuwa kiongozi mahiri ikiwemo uwezo wa kujenga na kutetea hoja, amefariki jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi la Wanachi wa Tanzania (JWTZ), Lugalo, Dar es Salaam.
Taarifa zimesema Mama Hawa Ngurume amefariki kutokana na ugonjwa wa Saratani, figo na vichomi.
Pia Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ametuma salamu zake za pole ambapo amesema Marehemu Hawa Ngulume, enzi za uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia maamuzi yake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo katika sehemu zote alizotumikia akiwa Mtumishi wa Umma, na baadaye alipopewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya alioutumikia katika Wilaya za Singida Mjini katika Mkoa wa Singida, Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na mara ya mwisho katika Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya.
“Nilimfahamu Marehemu, enzi za uhai wake, kama Kiongozi Mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake, na hivyo kuthibitisha ukweli kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza”, amesema Rais Kikwete katika kuomboleza kifo chake.
Akithibitisha habari hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Lugimbana amesema kuwa taarifa za mazishi zitatolewa baada ya kikao cha familia kupanga utaratibu kamili.

No comments:

Post a Comment