Waziri Wa Fedha Dkt Mgimwa akiwakilisha hotuba ya bajeti. |
I UTANGULIZI:
1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako
Tukufu liweze kujadili na kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali
kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na hotuba hii, nimewasilisha vitabu
vinne vya Bajeti vinavyoelezea takwimu mbalimbali za Bajeti. Kitabu cha Kwanza
kinaelezea makisio ya mapato. Kitabu cha Pili kinaelezea
makisio ya matumizi ya kawaida kwa Wizara, Idara zinazojitegemea; Taasisi na
Wakala wa Serikali; cha Tatu kinahusu makisio ya matumizi ya kawaida kwa
Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na cha Nne kinaelezea makadirio ya
matumizi ya maendeleo kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za
Serikali; Mikoa na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2012 ambao ni sehemu ya Bajeti hii.
2. Mheshimiwa
Spika, awali ya yote, naomba nitumie fursa
hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa aliyonayo kwangu kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Naahidi kutekeleza majukumu niliyokabidhiwa kwa umakini na uaminifu mkubwa.
3.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza wafuatao kwa
kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa mawaziri kama ifuatavyo: Mhe. Prof. Sospeter
Mwijarubi Muhongo (Mb); Mhe. Mhandisi Christopher Kajoro Chiza (Mb); Mhe. Dkt.
Harrison George Mwakyembe (Mb); Mhe. Dkt. Fenella Ephraim Mukangara (Mb); Mhe.
Balozi Khamis Sued Kagasheki (Mb); Mhe. Dkt. Abdallah Omari Kigoda (Mb). Aidha,
napenda kuwapongeza wafuatao kwa kuteuliwa kuwa naibu mawaziri katika Wizara
mbalimbali, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb); Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb); Mhe.
Dkt. Seif Suleiman Rashid (Mb.); Mhe. George Boniface Simbachawene (Mb.);
Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.); Mhe. Dkt. Charles John Tizeba (Mb.);
Mhe. Amos Gabriel Makalla (Mb.); Mhe. Angela Jasmine Kairuki (Mb.); Mhe.
Stephen Julius Maselle (Mb.); na Mhe. Mhandisi Dkt. Binilith Satano Mahenge
(Mb). Kadhalika, nampongeza Mhe. James Mbatia (Mb) kwa kuteuliwa na Mhe. Rais
kuwa Mbunge.
BOFYA HAPA CHINI KUENDELEA
4.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia, Mhe. Alhaji Adam Kimbisa (Mb.); Mhe. Shy Rose
Banji (Mb.); Mhe. Abdulah Alli Hassan Mwinyi (Mb); Mhe. Charles Makongoro
Nyerere (Mb); Mhe. Dkt Twaha Issa Taslima (Mb); Mhe. Nderkindo Perpetua Kessy
(Mb); Mhe. Bernard Musomi Murunyana (Mb); Mhe. Anjela Charles Kizigha (Mb.);
Mhe. Maryam Ussi Yahaya (Mb.), ambao wamechaguliwa kutuwakilisha kwenye Bunge
la Afrika Mashariki. Ni matumaini yangu watatuwakilisha vyema kwa maslahi na
manufaa ya Taifa letu.
5.
Mheshimiwa Spika, maandalizi
ya Bajeti hii yamehusisha wadau na Taasisi mbalimbali. Napenda kuwashukuru
walioshiriki kwa namna moja au nyingine kufanikisha matayarisho yake. Kwa namna
ya pekee, ninaishukuru Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi chini ya uenyekiti wa
Mhe. Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, pamoja na kamati
nyingine za kisekta kwa ushauri mzuri waliotoa wakati wakichambua mapendekezo
ya Bajeti hii. Aidha, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri na
mapendekezo yao ambayo yamezingatiwa katika Bajeti hii.
6.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mhe. Stephen
Masatu Wasira (Mb), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa ushirikiano
alionipatia wakati wa maandalizi ya Bajeti. Aidha, nawashukuru Naibu Mawaziri
wa Fedha, Mhe. Janet Zebedayo Mbene (Mb) na Mhe. Saada Mkuya Salum (Mb).
Namshukuru Katibu Mkuu Ndugu Ramadhani M. Khijjah; Naibu Katibu Wakuu, Ndugu
Laston T. Msongole; Dkt. Servacius B. Likwelile; na Ndugu Elizabeth Nyambibo
kwa mchango wao mkubwa katika matayarisho ya Bajeti. Vilevile, nawashukuru
Prof. Benno Ndulu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania;
Dkt. Phillip Mpango, Katibu
Mtendaji Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango; Ndugu Harry Kitilya, Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania; na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Takwimu ya Taifa. Nawashukuru wote kwa mchango wao katika maandalizi ya bajeti
hii. Naishukuru pia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa
wakati Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2012 na nyaraka mbalimbali za sheria
ambazo ni sehemu ya Bajeti hii.
7.
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Wakuu wa Idara,
Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na wafanyakazi wote wa Wizara
ya Fedha kwa ushirikiano wao. Aidha, namshukuru Mpigachapa Mkuu wa Serikali kwa
kuchapisha Hotuba hii kwa wakati. Nawashukuru pia wataalamu na wale wote
waliotoa mapendekezo kuhusu sera, mikakati na masuala mbalimbali ya kodi ambayo
yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti hii.
8.
Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa mwenyeji wa
Mikutano ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa Mwaka 2012
iliyofanyika kuanzia tarehe 28 Mei hadi tarehe 2 Juni 2012 na kufunguliwa rasmi
na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mikutano hii ilifanyika kwa ufanisi mkubwa katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 2,350 kutoka ndani na nje ya
Tanzania. Hii imekuwa ni nafasi ya kipekee kwa Tanzania kutangaza fursa
mbalimbali za kiuchumi zilizopo nchini. Aidha, washiriki wa ndani kutoka sekta
binafsi walipata nafasi ya kufahamu fursa za mikopo zilizopo katika Benki ya
Maendeleo ya Afrika. Napenda kutoa wito kwa sekta binafsi kutumia fursa hizo
kikamilifu.
9.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13 imelenga
kukabiliana na changamoto zinazokabili uchumi ikiwa ni pamoja na; kuongeza
fursa za kukuza uchumi, kushughulikia uhaba wa chakula nchini, kupambana na
mfumuko wa bei, kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kusimamia
matumizi, kushughulikia suala la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, kuwekeza
katika miundombinu ya nishati ya umeme hususan ujenzi wa bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam, barabara, bandari na reli ya kati ili kupunguza
gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika uzalishaji; pamoja na
kulipa madeni ya ndani na nje.
II. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA
SERA ZA BAJETI YA
MWAKA 2011/12
10.
Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba
sasa kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Mfumo wa Bajeti
ya mwaka 2011/12 uliendeleza juhudi za Serikali za kufikia malengo ya Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2025. Aidha, bajeti ilizingatia utekelezaji wa vipaumbele
vya Mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16); Awamu ya
Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA II); Malengo
ya Maendeleo ya Milenia 2015; Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA);
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Mkakati wa Taifa wa Madeni; pamoja na
kuimarisha usimamizi wa kodi na matumizi ya fedha za Umma.
11.
Mheshimiwa Spika, misingi
na shabaha za bajeti ya mwaka 2011/12, pamoja na mambo mengine, ililenga
kukamilisha malengo ya Serikali ya kukabiliana na changamoto za kupunguza
makali ya maisha kwa wananchi; kuendelea kuboresha mfumo wa makusanyo ya mapato
ya ndani; kuboresha mazingira ya uwekezaji wa ndani na nje; kuendeleza sekta
binafsi ili kupanua wigo wa kodi; kukamilisha maandalizi ya Mradi wa
Vitambulisho vya Taifa; na kutenga rasilimali na kutekeleza miradi katika
maeneo ya kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
12.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengine
yaliyozingatiwa katika misingi na shabaha ya bajeti hiyo yalikuwa ni: kutekeleza
mipango na mikakati maalum ya kuharakisha ukuaji wa uchumi; kutafuta mikopo ya
masharti nafuu na ya kibiashara; kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Ubia kati
ya Sekta ya Umma na ya Binafsi ili kupanua fursa za utekelezaji wa miradi ya
maendeleo; Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012; kuhakikisha kwamba maduhuli
ya Serikali yanakusanywa ipasavyo na kuwasilishwa katika Mfuko Mkuu wa
Serikali; pamoja na kulinda na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta
za huduma za jamii, hususan elimu na afya ambazo zimekuwa na upanuzi mkubwa wa
huduma.
Hatua za Utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12
Kupunguza Makali ya Maisha
13.
Mheshimiwa Spika, katika
utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/12, Serikali iliendelea kuchukua hatua
mbalimbali kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi kwa lengo la
kupunguza makali ya maisha kunakotokana na kupanda kwa bei za bidhaa na huduma.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na: kurekebisha namna ya kukokotoa gharama za
mafuta na kutangaza bei elekezi kila mwezi na kuanzisha utaratibu wa uagizaji
mafuta kwa pamoja (bulk procurement). Hatua hizi zimesaidia kupunguza kasi ya
upandaji wa bei ya mafuta hapa nchini.
14.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imetumia shilingi bilioni 296 kutekeleza mpango wa dharura wa kukabiliana na
tatizo la upungufu wa nishati ya umeme kwa kutumia mitambo ya kukodi.
Utekelezaji wa jitihada hizi umeongeza megawati 324 kwenye Gridi ya Taifa.
Kadhalika, Serikali ilitumia Dola za Marekani milioni 183 kugharamia ujenzi wa
mitambo ya kufua umeme wa megawati 100 kwa mkoa wa Dar es Salaam mradi ambao
umekamilika na uko kwenye hatua za majaribio na Megawati 60 kwa mkoa wa Mwanza
ambao bado ujenzi unaendelea.
15.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imetumia shilingi bilioni 27 kugharamia ununuzi na usambazaji wa tani 120,000
za mahindi katika masoko kwa lengo la kukabiliana na uhaba wa chakula kwa
baadhi ya maeneo. Aidha, Serikali ilitoa vibali vya kuagiza sukari bila kutoza
ushuru wa forodha kiasi cha tani 200,000 ili kukabiliana na uhaba na kupanda kwa
bei ya sukari. Kadhalika, Serikali ilipandisha kiwango cha riba inayotozwa na
Benki Kuu kwa Taasisi za Fedha kutoka asilimia 7.58 hadi asilimia 12.58.
Vilevile, Serikali ilipandisha kiwango cha amana ambacho benki za biashara
zinapaswa kuhifadhi Benki Kuu kutoka asilimia 20 hadi asilimia 30. Hatua hizi
zimesaidia kupunguza kasi ya kupanda kwa bei.
Kuwezesha
Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira
16.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na tatizo la
ajira, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuongeza fursa za ajira. Hatua
hizo ni pamoja na: kuboresha mazingira ya kisera na kisheria kuwezesha sekta
binafsi kukua; kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuongeza mitaji
katika Benki ya Rasilimali, Benki ya Wanawake, Benki ya Posta na Twiga Bancorp,
na kufanikisha uanzishwaji wa kampuni ya kutoa mikopo ya muda mrefu ya ujenzi
wa nyumba na makazi. Hatua nyingine zilizochukuliwa na kuchangia ongezeko la
ajira ni pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo, mawasiliano
na kuwezesha wananchi kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji. Aidha, kuna
Taasisi mbalimbali ambazo zimechangia kutoa ajira kama vile, TASAF, SELF, VETA,
Shirika la Viwanda Vidogovidogo (SIDO), Taasisi ndogondogo za Fedha, VICOBA,
Benki za Kijamii na Mifuko ya Udhamini ya mikopo inayosimamiwa na Benki Kuu.
Katika mwaka 2011/12, Serikali iliajiri Walimu wa Shule za Sekondari na Msingi
25,000, Maafisa Ugani wa Kilimo na Mifugo 4,499 na Watumishi wa Kada ya Afya
6,916.
Uboreshaji
wa Mazingira Wezeshi kwa Sekta Binafsi
17.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza utekelezaji wa
Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Uwekezaji mwaka 2011 kufuatia kuidhinishwa
kwake mwaka 2010. Kupitia Mpango huu, taratibu na kanuni za mawasilisho na
malipo ya kodi na ushuru yanafanyika kwa njia ya mtandao. Utaratibu huu
umeongeza ufanisi kwa kuondoa usumbufu na upotevu wa muda katika ulipaji wa
kodi. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 75 ya walipa kodi wakubwa na walipa kodi
wengine 2,795 wanafanya mawasilisho yao kwa njia ya mtandao. Aidha,
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania ilianzisha mfumo unaounganisha
usimamizi wa kodi (Asycuda, ITAX) na benki za biashara ili kurahisisha ulipaji
wa kodi. Mfumo huu umeunganisha jumla ya benki 25. Kadhalika,
Mamlaka inatumia huduma za M-Pesa (Vodacom) na “NMB mobile” kwa ajili ya
kulipia kodi ya majengo na kodi ya mapato.
18.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na jitihada za
kupunguza urasimu katika utoaji wa mizigo bandarini kwa kuanzisha utaratibu wa
kuwasilisha nyaraka kwa njia ya mtandao kabla ya mizigo kuwasili. Utaratibu huu
umelenga kupunguza tatizo la mrundikano na upotevu wa nyaraka na kupelekea
kupungua kwa muda na gharama za uagizaji na usafirishaji mizigo nje ya nchi.
Serikali imepunguza vizuizi vya usafirishaji mizigo ndani ya nchi kutoka
50 vilivyokuwepo kufikia 15, isipokuwa vituo vya mizani na forodha. Lengo la
hatua hii ni kupunguza gharama za kufanya biashara na usumbufu wanaopata
wafanyabiashara.
Sera za Mapato
19.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2011/12, Serikali iliendelea kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani
yanayotokana na kodi na yasiyo ya kodi kwa kuchukua hatua za kiutawala, kisera
pamoja na marekebisho ya viwango vya kodi na sheria.
20.
Mheshimiwa Spika, Serikali
ilifanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ili
kuboresha uzalishaji katika sekta za Kilimo, Mifugo, Viwanda, Biashara na
Utalii. Marekebisho hayo ni pamoja na kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani
kwenye vipuri vya zana za kilimo; chakula cha kukuzia kuku; nyuzi za
kutengenezea nyavu za kuvulia samaki; pamoja na kuanzisha utaratibu wa
kuwarejeshea kodi wageni kwa bidhaa walizonunua nchini wakati wanaondoka.
21.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilifuta msamaha wa Kodi
ya Ongezeko la Thamani kwenye kuuza na kupangisha majengo ya nyumba za kuishi
za Shirika la Nyumba la Taifa - NHC; kuondoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la
Thamani kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali isipokuwa kwenye vifaa vya misaada
kwa vituo vya kulelea watoto yatima na shule.
22.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia
ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332 kwa kufuta kodi ya
Zuio kwa usafirishaji wa samaki nje ya nchi ili kuongeza utoaji wa huduma za
usafirishaji wa mazao ya samaki kutokea hapa nchini badala ya kupitia nchi za
jirani. Aidha, marekebisho yalifanyika katika Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA
147 kwa kupunguza ushuru wa bidhaa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo
ili kupunguza gharama za uzalishaji.
23.
Mheshimiwa Spika, Sheria ya
Ushuru wa Mafuta ya Petroli, SURA 220 ilifanyiwa marekebisho kwa kutoa msamaha
wa ushuru unaotozwa kwenye mafuta yanayotumika katika kuendesha meli, na vifaa
vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili kupunguza gharama.
Aidha, marekebisho yalifanyika kwenye Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki, ya mwaka 2004 kufuatia kuridhia kwa Mawaziri wa Fedha
wa Nchi Wanachama kufanya marekebisho mbalimbali katika kukuza Sekta za
Viwanda, Usafirishaji, Mifugo, Biashara na Utalii. Vilevile, marekebisho yalilenga
katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali
zao.
24.
Mheshimiwa Spika, hatua
nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuhamasisha na kuhakikisha
mashine za kielectroniki – EFD zinatumika ipasavyo; kuimarisha mfumo wa
kusimamia vitalu vya kodi; kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa wateja na vya
kukusanyia mapato; kuimarisha mifumo ya malipo ya kodi; na kuboresha mfumo wa
uthaminishaji kwa kuimarisha ukaguzi wa hesabu za walipa kodi.
Mwenendo wa
Ukusanyaji Mapato
25.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa
fedha 2011/12, Serikali ilipanga kukusanya mapato ya jumla ya shilingi bilioni
13,525.9 kutoka katika vyanzo mbalimbali na kutumia kiasi hicho kwa matumizi ya
kawaida na maendeleo. Vyanzo vya mapato vilikuwa kama ifuatavyo: mapato ya
ndani yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 6,775.9; mapato kutoka
Serikali za mitaa yalikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 350.5;
misaada na mikopo ya kibajeti ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni
869.4; misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo na ya kisekta ilikadiriwa
kufikia kiasi cha shilingi bilioni 3,054.1; mikopo ya ndani na nje yenye
masharti ya kibiashara ilikadiriwa kufikia kiasi cha shilingi bilioni 1,664.9;
na mikopo ya kulipia dhamana na hatifungani zinazoiva zilikadiriwa kufikia
kiasi cha shilingi bilioni 810.9.
26.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri, hadi Aprili 2012 makusanyo
yamefikia jumla shilingi bilioni 5,684.5. Kiasi hiki ni sawa na asilimia 80 ya
makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 7,126.4 kwa mwaka 2011/12.
27.
Mheshimiwa Spika, makusanyo ya
kodi yalifikia shilingi bilioni 5,227.5 ambayo ni sawa na asilimia 84 ya
makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 6,228.8. Kulingana na mwenendo wa
makusanyo ya mapato ya kodi kwa kipindi cha miezi kumi ya mwaka 2011/12, hadi
kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha 2011/12 Serikali inatarajia kukusanya jumla
ya shilingi bilioni 6,307.8 na hivyo kuweza kufikia lengo tulilojiwekea.
28.
Mheshimiwa Spika, mapato
yasiyotokana na kodi yamefikia shilingi bilioni 451.6 ikiwa ni asilimia 83 ya
lengo la kukusanya shilingi bilioni 547.1 kwa mwaka. Kutokana na mwenendo huo,
Serikali inatarajia hadi Juni 2012 kufikia lengo.
29.
Mheshimiwa Spika, mapato ya
Serikali za Mitaa yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 143, sawa na asilimia
40.8 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 350.5 kwa mwaka. Hadi Juni 2012,
Serikali inatarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 200 kutokana na chanzo
hiki ikiwa ni asilimia 57 ya lengo la mwaka. Kutokufikia malengo ya ukusanyaji
wa mapato haya kumechangiwa na kuchelewa kuanza kutekeleza utozaji wa ada za
leseni.
Misaada
na Mikopo ya Masharti Nafuu Kutoka Nje
30.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12, Serikali
ilikadiria kupata kiasi cha shilingi bilioni 869.4 kama misaada na mikopo ya
kibajeti ambapo hadi sasa Serikali imepokea shilingi bilioni 916.3, ikiwa zaidi
kwa shilingi bilioni 46.9. Ongezeko hili limetokana na baadhi ya wafadhili
kutoa fedha zaidi ya kiwango walichoahidi. Kwa upande wa misaada na mikopo ya
miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya kisekta, hadi kufikia Aprili 2012
ilifikia shilingi bilioni 1,450.4 sawa na asilimia 47 ya makadirio ya bajeti ya
mwaka ya shilingi bilioni 3,054.1. Upungufu huu umesababishwa na kasi ndogo ya
utekelezaji wa baadhi ya miradi na kuchelewa kupokea taarifa ya fedha hizi
kutoka kwa washirika wa maendeleo na Wizara na Taasisi zinazotekeleza miradi
husika.
Mikopo
ya Ndani
31.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi
cha Julai 2011 hadi Aprili 2012, Serikali imekopa kiasi cha shilingi bilioni
526 kwa ajili ya kulipia dhamana za Serikali zilizoiva ikiwa ni asilimia 64 ya
lengo la mwaka la shilingi bilioni 819.1. Aidha, Serikali ilipanga kukopa
shilingi bilioni 393.4 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa kwa ajili ya
kugharamia matumizi ya maendeleo. Hadi kufikia Aprili 2012, Serikali ilikuwa
imekopa shilingi bilioni 232.6 sawa na asilimia 59 ya makadirio ya mwaka.
Mikopo ya Nje yenye Masharti ya
Kibiashara
32.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/12
Serikali ilikadiria kukopa kiasi cha Dola za Marekani milioni 822, sawa na
shilingi bilioni 1,271.6 kama mikopo ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai
2011 hadi Aprili 2012, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa kiasi cha Dola za Marekani
milioni 310 na Benki ya Standard ya Afrika Kusini. Hadi kufikia Aprili 2012,
jumla ya Dola za Marekani milioni 229 ambazo zilitumika kulipia madeni
ya barabara ya mwaka 2010/11. Aidha, Serikali ilisaini Mkataba wa mkopo wa Euro
milioni 61 na Benki ya HSBC. Mkopo huu umeelekezwa kugharamia ujenzi wa mtambo
wa kufua umeme wa megawati 60 Nyakato Mwanza. Serikali pia imesaini mkataba wa
mkopo wa Dola za Marekani milioni 350 kutoka Benki ya Credit Suisse ya
Uingereza ambapo Dola za Marekani milioni 200 zimepokelewa mwanzoni mwa Mwezi
Juni 2012. Kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 150 kitapatikana
na kutumika mwaka 2012/13.
33.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imepata Mshauri Mwelekezi ambaye ataishauri Serikali katika zoezi la kujiandaa
kufanyiwa tathmini ya uwezo wa kukopa na kulipa madeni (Sovereign Credit
Rating). Maandalizi haya yataiwezesha nchi kufanyiwa tathmini
yanatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2013. Kukamilika kwa zoezi hilo
kutawapatia wakopeshaji imani na hivyo kuiwezesha Serikali kupata mikopo yenye
masharti nafuu ya kibiashara kwa wakati.
Sera za Matumizi
34.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2011/12, Serikali iliendelea kutekeleza sera za matumizi kulingana na
upatikanaji wa mapato ya ndani, misaada pamoja na mikopo ya ndani na nje.
Aidha, Serikali iliendelea kuboresha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha
za umma, ikijumuisha udhibiti wa ulipaji wa mishahara, matumizi katika miradi
ya maendeleo, ruzuku ya pembejeo, ununuzi wa umma na kuendelea kudhibiti
malimbikizo ya madeni. Serikali imeandaa mkakati wa kulipa na kudhibiti madeni
yatokanayo na malimbikizo ya madai ya watumishi; wakandarasi; wazabuni; na
madeni mengineyo. Madeni hayo yatalipwa baada ya kuhakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa
Ndani.
Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma
35.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuimarisha
usimamizi wa fedha za umma, Serikali iliendelea kutekeleza programu ya
maboresho ya usimamizi wa fedha za umma katika Serikali Kuu na Serikali za mitaa.
Katika utekelezaji wa programu hiyo Serikali imeweka mtandao wa IFMS katika
Halmashauri 133. Aidha, Serikali imetoa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo
ya kibenki - TISS kwa watumishi wa kada ya Uhasibu katika mikoa
20, Hazina ndogo zote, Ofisi ya Bunge, TAMISEMI na Ofisi ya Mrajisi wa vyama
vya Ushirika. Vilevile, Serikali imetoa mafunzo kwa Wahasibu wa Wizara,
Idara, Mikoa na Balozi zetu 32 katika kuandaa Hesabu za Serikali kwa viwango
vya Kimataifa (IPSAS – Accruals basis).
36.
Mheshimiwa Spika, kutokana na maboresho hayo,
usimamizi wa fedha katika Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa na Mamlaka ya Serikali
za Mitaa unaendelea kuimarika. Hali hii inajidhiirisha katika taarifa ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/11 ambapo Hati
safi za ukaguzi kwa Wizara, Idara na Sekretarieti za Mikoa zimeongezeka kutoka
asilimia 71 hadi asilimia 85. Wakati Hati zenye shaka zimepungua kutoka
asilimia 26 mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 15 kwa mwaka wa fedha 2010/11
na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha ikilinganishwa na mwaka 2009/10 ambapo
Hati hizo zilitolewa kwa Taasisi mbili.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Balozi zetu Hati safi
zimeongezeka kutoka asilimia 71 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 85 mwaka
2010/11 na hapakuwepo na Hati zisizoridhisha katika mwaka 2010/11. Aidha,
kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa Hati safi zimeongezeka kutoka asilimia 49
mwaka wa fedha 2009/10 hadi asilimia 54 mwaka 2010/11 na Hati zenye shaka
zimepungua kutoka asilimia 64 mwaka 2009/10 na kufikia asilimia 56 mwaka
2010/11.
38.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2011/12, Serikali imefungua akaunti sita kwa kila Halmashauri kwa ajili ya
uendeshaji wa majukumu yao. Akaunti hizo ni za Mapato; Amana; Matumizi ya
kawaida; Mishahara; Maendeleo; na Mfuko wa Barabara. Lengo la hatua hii ni
kupunguza gharama za uendeshaji, urasimu wa matumizi, ugumu wa kutoa taarifa za
matumizi, ulimbikizaji wa fedha kwenye akaunti bila kutumika kwa muda mrefu na
kudhibiti fedha zisitumike katika shughuli ambazo hazikuidhinishwa.
Mwenendo wa Matumizi
39.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
matumizi, Serikali ilikadiria kutumia kiasi cha shilingi bilioni 13,525.9
katika mwaka wa fedha wa 2011/12. Mgawanyo wa matumizi ya Serikali katika
kipindi hiki ulikuwa kama ifuatavyo; kiasi cha shilingi bilioni 8,600.3
zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 4,925.6
zilikadiriwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Matumizi ya kawaida
40.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi
cha Julai 2011 hadi Aprili 2012 matumizi ya kawaida yamefikia
shilingi bilioni 7,349.8 sawa na asilimia 85.5 ya makadirio ya mwaka kama
ilivyo katika ridhaa ya matumizi. Kati ya kiasi hicho, malipo ya mishahara ya
watumishi wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka ya Serikali za Mitaa,
Taasisi na Mashirika ya Umma yalikuwa shilingi bilioni 2,760.5 sawa na asilimia
84.4 ya lengo la mwaka la shilingi bilioni 3,270.3. Malipo ya
riba kwa mikopo ya ndani na nje yalikuwa shilingi bilioni 316.1 sawa na
asilimia 102.4 ya makadirio ya shilingi bilioni 308.7 kwa mwaka. Malipo ya
mikopo ya nje yalikuwa shilingi bilioni 57.3 sawa na asilimia 85.7 ya makadirio
kwa mwaka. Serikali ilitumia shilingi bilioni 526 kwa ajili ya kulipia dhamana
za Serikali za muda mfupi na Hatifungani za Serikali zilizoiva. Serikali
imeendelea kutoa kipaumbele katika kulipa madeni kwa wakati ili kuepuka
malimbikizo ya riba.
41.
Mheshimiwa Spika, matumizi
mengineyo katika Wizara, Idara, Taasisi za Serikali, Mikoa na Halmashauri
yalifikia shilingi bilioni 2,384.9 ikiwa ni asilimia 72.8 ya makadirio ya
shilingi bilioni 3,275.1 kwa mwaka. Kati ya matumizi mengineyo, kiasi cha
shilingi bilioni 284.1 zilitumika kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya
juu ikiwa ni asilimia 89 ya bajeti ya mwaka ya shilingi bilioni 317.4, na hivyo
kunufaisha jumla ya wanafunzi 93,176. Kadhalika, Serikali ililipa kiasi cha
shilingi bilioni 44.0 za madai ya walimu wa shule za msingi na sekondari
yaliyohakikiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ndani.
Matumizi ya Maendeleo
42.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa
Matumizi ya Maendeleo kiasi cha shilingi bilioni 2,657.2 ziligharamia miradi ya
maendeleo ikilinganishwa na makadirio ya mwaka ya kutumia shilingi bilioni
4,924.6. Fedha za ndani zilikuwa shilingi bilioni 1,201.6 ikilinganishwa na
makadirio ya mwaka ya shilingi bilioni 1,871.5 sawa na asilimia 64.2. Upungufu
huu umetokana na kuchelewa kupatikana kwa wakati kwa mikopo ya nje yenye
masharti ya kibiashara. Jumla ya shilingi bilioni 663.8 ziligharamia miradi ya
miundombinu, kati ya hizo shilingi bilioni 296 zilitumika kwenye miradi ya
umeme na shilingi bilioni 367.8 kwenye miradi ya barabara. Matumizi ya
maendeleo yaliyogharamiwa kwa fedha za nje yalikuwa shilingi bilioni 1,450.4
ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 3,054.1 sawa na asilimia 47.
Vitambulisho
vya Taifa na Anwani za Makazi
43.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na azma
yake ya kutekeleza mradi wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia, pamoja
na mambo mengine, kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja
na huduma za kifedha. Mradi huu unaenda sambamba na uanzishwaji wa anwani za
makazi. Vitambulisho hivyo vitaanza kutolewa katika robo ya kwanza ya mwaka
2012/13 kwa Zanzibar na Mkoa wa Dar es Salaam.
Sensa ya Watu na Makazi na Utafiti Kuhusu Hali ya Umaskini
44.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Sensa ya
Watu na Makazi Serikali imeendelea kugharamia maandalizi ya Sensa ya Watu na
Makazi, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95. Hadi sasa Serikali imetumia
shilingi bilioni 23.6 kugharamia maandalizi ya zoezi la Sensa. Sensa hiyo
imepangwa kufanyika tarehe 26 Agosti 2012. Aidha, Serikali iliendelea
kugharamia utafiti wa mapato na matumizi katika kaya. Utafiti huu ulianza mwezi
Oktoba 2011, na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2012 na matokeo
yanatarajiwa kutoka mwezi Julai 2013. Utafiti huu utatoa picha halisi ya hali
ya umaskini, hususan wa kipato tangu mwaka 2007 hadi mwaka 2012. Hii itasaidia
kutambua mwenendo wa umaskini wa kipato na sababu zilizopelekea mwenendo huo.
Utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II)
45.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi
cha mwaka 2011/12, serikali iliendelea kutekeleza MKUKUTA awamu ya pili
unaojielekeza katika maeneo ya kukuza uchumi na kupunguza umaskini wa kipato,
kuboresha maisha na ustawi wa jamii, na utawala bora na uwajibikaji sambamba na
Melengo ya Maendeleo ya Milenia. Ili kufikia matokeo tarajiwa katika kila eneo,
sekta kadhaa huchangia katika utekelezaji kupitia sera, mikakati na mipango ya
kisekta. Kwa mantiki hiyo, utekelezaji wa MKUKUTA II
unahitaji ushirikiano wa sekta mbalimbali za uchumi katika hatua ya upangaji na
utekelezaji.
46.
Mheshimiwa Spika, MKUKUTA ni
mkakati unaoziweka pamoja juhudi za Serikali na wadau mbalimbali
katika kupambana na umaskini. Aidha, umaskini ni suala pana linalojumuisha
umaskini wa kipato na usio wa kipato. Ni kweli kuwa umaskini wa kipato umekuwa
ukipungua kwa kasi ndogo. Hata hivyo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za
kupunguza umaskini kwa kujenga mazingira bora ili wananchi washiriki kikamilifu
katika shughuli za uchumi, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika elimu, afya,
miundombinu na sekta ya fedha.
47.
Mheshimiwa Spika, pamoja na
changamoto zilizojitokeza, hususan mtikisiko wa uchumi duniani, uchumi
uliendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Kiwango cha ukuaji wa uchumi kwa
mwaka 2011, kilikuwa asilimia 6.4 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2010.
Aidha, pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka shilingi 770,464 kwa mwaka
2010 hadi shilingi 869,436 kwa mwaka 2011. Kwa wastani, ongezeko hili
limeongeza uwezo wa wananchi kupata huduma bora ikiwa ni pamoja na nyumba bora,
simu za mkononi, pikipiki na usafiri wa baiskeli.
48.
Mheshimiwa Spika, Serikali
iliendelea kutekeleza programu mbalimbali za huduma ya jamii kwa lengo la
kuboresha maisha na ustawi wa jamii. Matokeo ya utekelezaji wa programu hizo
zinaonesha mabadiliko chanya. Katika sekta ya elimu, viwango vya uandikishaji
na kumaliza katika ngazi zote za elimu vinaridhisha. Mfano, kiwango cha
uandikishwaji katika elimu ya msingi, kilikuwa asilimia 94 na katika elimu ya
sekondari ni asilimia 35 kwa mwaka 2011. Huduma za afya kwa mtoto na mama
zinaendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa mpango wa afya ya mtoto na
mama. Aidha, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama
imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa programu ya sekta ya maji
iliyoanza mwaka 2007.
49.
Mheshimiwa Spika, katika
kudumisha utawala bora na uwajibikaji, Serikali iliendelea kuchukua hatua
mbalimbali ikiwa ni pamoja na: kuimarisha sekta ya sheria kwa kuongeza idadi ya
mahakimu wa Mahakama za mwanzo; kuimarisha mfumo wa sheria na haki za binadamu;
kuhamasisha umma kuhusu haki za binadamu na wajibu wa jamii; na kushiriki katika
mpango wa nchi za Afrika kujitathmini zenyewe katika masuala ya utawala bora.
Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha za umma, kwa
kuimarisha ofisi za ukaguzi katika wizara, mikoa na Mamlaka za Serikali za
Mitaa.
Sekta ya Fedha
50.
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya mageuzi mbalimbali
katika sekta ya fedha ili kuhakikisha kwamba inachangia kikamilifu katika
shughuli za kiuchumi na kukuza Pato la Taifa. Mageuzi haya yameleta mafanikio
makubwa.Hadi kufika mwezi Aprili mwaka 2012 idadi ya benki imeongezeka na
kufikia 49 kutoka benki 43 Aprili mwaka 2011. Kadi za simu za mkononi
zinazotumika kutoa huduma za kifedha zimefikia 21,184,808 mwaka 2011 kutoka
10,663,623 mwaka 2010. Aidha, idadi ya Taasisi ndogo ndogo za kifedha
zimefikia 150 mwaka 2011.
51.
Mheshimiwa Spika, Serikali
iliendelea kutoa Mikopo ya kilimo kupitia dirisha la Kilimo lililopo katika
Benki ya Rasilimali Tanzania. Hadi kufikia Machi, 2012 jumla ya mikopo 81 yenye
thamani ya shilingi bilioni 22.9 ilitolewa, kati ya mikopo hiyo, 42 ni ya
SACCOS, 32 ni kwa ajili ya makampuni na 7 kwa Taasisi ndogondogo za fedha
(MFIs). Mikopo iliyotolewa kwa MFIs na SACCOS ilitumika kukopesha miradi mingi
ya wakulima wadogo wadogo vijijini. Aidha, Serikali imetoa shilingi bilioni 30
kwa ajili ya mtaji wa Benki ya Kilimo.
52.
Mheshimiwa Spika, Serikali iliendelea na utekelezaji
wa programu ya mageuzi na maboresho ya Ushirika nchini ili kuimarisha vyama
vikuu vya ushirika na kuviwezesha kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wengi
zaidi hususan waliopo vijijini. Mwaka 2011, idadi ya Vyama vya Ushirika wa
Akiba na Mikopo (SACCOS) iliongezeka na kufikia 5,346 kutoka vyama 5,314 mwaka
2010. Vile vile, idadi ya wanachama iliongezeka kwa asilimia 5.7 na kufikia
wanachama 970,655 kutoka wanachama 917,889 mwaka 2010. Aidha, Hisa, Akiba na
Amana za wanachama ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 236.8 mwaka 2010 hadi
shilingi bilioni 399.0 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 68.5. Mikopo
iliyotolewa kwa wanachama iliongezeka kutoka shilingi bilioni 539.2 mwaka 2010
hadi shilingi bilioni 627.2 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia
16.3.
53.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia
Machi 2012, mikopo kwa sekta binafsi iliongezeka kwa asilimia 21.9
ikilinganishwa na asilimia 23.3 Machi 2011. Ongezeko hili linaenda sambamba na
kuongezeka kwa rasilimali za fedha za ndani kwenye benki pamoja na kupungua kwa
ukuaji wa rasilimali za fedha za kigeni kwenye benki. Sehemu kubwa ya mikopo
hii ilielekezwa katika shughuli binafsi asilimia 21.9; biashara asilimia 19.9;
uzalishaji bidhaa viwandani asilimia 11.9; kilimo asilimia 11.8; na usafiri na
mawasiliano asilimia 7.9.
54.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza
upatikanaji wa mikopo, Serikali imepata Mshauri Mwelekezi kwa ajili ya kuanzisha
taasisi ya kuratibu taarifa za wakopaji (Credit Rerefence Bureau) na mfumo wa
kuhifadhi taarifa za wakopaji (Credit Reference Databank). Mshauri mwelekezi
ameanza zoezi la kuweka mitambo na kutoa mafunzo kwa watumiaji. Aidha, Serikali
imeboresha mazingira ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na kati kwa ajili
ya nyumba, Kilimo na uwekezaji ambapo kanuni za taasisi za fedha za
maendeleo ziliandaliwa na kuchapishwa katika Gazeti la Serikali la Machi
2012.
55.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2011/12,
Serikali imeendelea kufanya maboresho katika sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa
kufanya tathmini ya uwekezaji wa mifuko, uhai wa mifuko, pamoja na kuandaa
mwongozo za uwekezaji wa mifuko hiyo. Aidha, Serikali imefanya marekebisho ya
Sheria za Mifuko yote pamoja na Mamlaka ya Usimamiaji wa Shughuli za Mifuko
(SSRA) ili kuboresha usimamizi wa mifuko hiyo.
Ubia
Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi
56.
Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu lilipitisha
sheria mpya ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2010 ili
kutoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa miundombinu na
kuiendesha kwa lengo la kutoa huduma bora za kijamii na kiuchumi kwa wananchi.
Katika mwaka 2011/12, Serikali imefanya maandalizi ya utekelezaji wa Sera ya Ubia
ikiwa ni pamoja na kuanzisha madawati ya PPP kwa kila Wizara na kuandaa
miongozo itakayotumika kuchambua na kuidhinisha miradi ya Ubia kwa mujibu wa
sheria. Aidha, Serikali imeanza hatua za awali kubaini miradi inayoweza
kutekelezwa kwa utaratibu wa Ubia kwa mujibu wa sheria.
57.
Mheshimiwa Spika, dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma
na Sekta Binafsi inatekelezwa kwa kutumia sheria mbili – Sheria ya Ubia ya
mwaka 2010 na Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2004 iliyorekebishwa mwaka
2011. Sababu za kurekebisha Sheria ya Ununuzi wa Umma pamoja na mambo mengine
ni kuingiza vifungu vinavyowezesha Taasisi za Serikali kupata Wabia makini wa
uwekezaji katika miradi ya Umma kwa njia zilizo wazi. Aidha, katika mwaka
2012/13, Serikali itakamilisha Kanuni za Sheria ya Ununuzi wa Umma ambazo
zinazingatia mazingira ya kipekee ya Sheria ya Ubia ambayo inawezesha kupata
Wabia walio tayari kuwekeza katika miradi husika. Serikali itahakikisha kanuni
na taratibu zote za kuidhinisha na kusimamia miradi ya ubia zinazingatiwa.
58.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/13,
Serikali itatoa mafunzo ya uelewa wa dhana ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na
Sekta binafsi kwa watumishi wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Taasisi za
Serikali, na Halmashauri zote. Aidha, Serikali itachagua miradi michache ya
kuanza nayo ili kupata uzoefu wa uendeshaji wa miradi hiyo. Maeneo
tunayotarajia kuanza nayo ni barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege, maji
pamoja na ujenzi wa ofisi.
59.
Mheshimiwa Spika, Napenda kutumia fursa hii kuziomba
Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika ya Umma, na Mamlaka ya Serikali za
Mitaa kuhamasisha Sekta Binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi
mbalimbali kwa kuzingatia taratibu na kanuni zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria.
Usimamizi wa Deni la Taifa
60.
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma yake ya
kuboresha miundombinu ya kimkakati, Serikali imeendelea kukopa kutoka nje na
ndani ya nchi ili kugharamia miradi mbali mbali ya maendeleo. Hadi mwishoni mwa
Machi 2012, deni la taifa lilikuwa shilingi bilioni 20,276.6 ikilinganishwa na
deni la shilingi bilioni 17,578.9 Machi 2011 ikiwa ni sawa na ongezeko la
asilimia 15.4. Kati ya hizo, shilingi bilioni 15.306.9 zilikuwa ni deni la nje
na shilingi bilioni 4,969.7 ni deni la ndani. Kati ya kiasi cha deni la
nje, shilingi bilioni 12,342.5 zilikuwa ni deni la umma na kiasi kilichobaki
cha shilingi bilioni 2,964.4 ni deni la sekta binafsi. Aidha, hadi kufikia
Machi 2012, deni la ndani la Serikali lilifikia shilingi bilioni 4,969.7 ikilinganishwa
na shilingi bilioni 4,496.5 mwezi Machi, 2011, sawa na ongezeko la asilimia
10.5. Sababu kubwa ya kuongezeka kwa deni la taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya
kugharimia miradi ya maendeleo na utumiaji wa dhamana za muda mfupi za Serikali
kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei katika uchumi na kushuka kwa thamani ya
shilingi kuliongeza deni la nje.
61.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Deni la
Taifa linasimamiwa vizuri, mwezi Februari, 2012, Serikali ilifanya tathmini ya
uhimilivu wa deni (Debt Sustainability Analysis) likijumuisha dhamana
zinazotolewa na Serikali kwa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma ambapo
matokeo ya tathmini hiyo yanaonesha kuwa Deni la Taifa linahimilika.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
62.
Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha Taasisi, Wakala na Mashirika ya umma yanatekeleza majukumu yao,
Serikali imetoa Waraka Na.1 wa mwaka 2012 unaoelekeza Wizara mama na
Bodi za Wakurugenzi kuingia katika mikataba ya utendaji, Waraka huo umeanza
kutumika Januari, 2012. Aidha, ukaguzi wa kiutendaji (Management Audit) katika
Taasisi za Serikali umefanyika kwa baadhi ya Taasisi na Mashirika ya umma kwa
kuangalia uzingatiaji wa kanuni, Sheria na miongozo mbalimbali inayotolewa na
Serikali ikiwa ni pamoja na uwajibikaji na utawala bora, matumizi ya fedha
na taratibu za ajira. Zoezi hili ni endelevu na linalenga kuboresha
uendeshaji wa Mashirika na Taasisi za Serikali. Kadhalika, Serikali imefanya
uhakiki wa mashirika 170 yaliyobinafsishwa. Kati ya hayo, mashirika 41 yalikutwa
yanajiendesha kwa faida, mashirika 66 yanajiendesha kwa hasara na mashirika 63
yalikuwa muflisi. Kwa yale ambayo yanaendeshwa kwa hasara yatawekwa chini ya
mfilisi kwa lengo la kuyachambua na kupendekeza hatua za kuchuliwa. Aidha, kwa
yale yaliyokuwa muflisi hatua za kuyafilisi zinaendelea.
III. BAJETI YA MWAKA 2012/13
63.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka
2012/13 itazingatia vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa
mwaka 2012/13; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini
(MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya
mwaka 2010 na program za maboresho katika sekta ya umma. Lengo likiwa ni
kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
64.
Mheshimiwa Spika, pamoja na
miongozo hiyo, Bajeti hii inazingatia pia changamoto zilizojitokeza wakati wa
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/12. Changamoto hizo ni pamoja na
upatikanaji wa umeme wa uhakika; kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la
Dunia; uhaba wa chakula katika baadhi ya maeneo; kupanda kwa bei za bidhaa na
huduma; kutopatikana kwa wakati fedha za kugharamia miradi ya maendeleo
kulikosababishwa na masharti magumu na urasimu kwa mikopo ya kibiashara; na
kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni ya ndani, hususan ya wazabuni, wakandarasi
na watumishi. Mambo mengine yaliyozingatiwa ni pamoja na mwenendo
wa uchumi wa dunia na makubaliano ya kikanda na kimataifa. Serikali imepanga
hatua mbalimbali za kuchukua kukabiliana na changamoto hizo kama nitakavyoeleza
hapo baadae.
Shabaha na Malengo ya Bajeti ya mwaka 2012/13
65.
Mheshimiwa Spika, Bajeti ya mwaka 2012/13,
imejielekeza katika kufikia Shabaha na malengo yafuatayo:
i.
Kukuza Pato halisi la Taifa kwa
asilimia 6.8 mwaka 2012 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 6.4 mwaka 2011;
ii.
Kuimarisha
miundombinu ya uchumi, ikijumuisha umeme, barabara, reli na bandari;
iii.
Kuongeza
upatikanaji wa huduma za kifedha;
iv.
Kuongezeka kwa
mapato ya ndani yatakayofikia uwiano na Pato la Taifa wa asilimia 18 kwa
mwaka 2012/13 kulinganisha na mwelekeo wa asilimia 16.9 mwaka 2011/12;
v.
Kuendelea
kudhibiti mfumuko wa bei ili urudi kwenye viwango vya tarakimu moja;
vi.
Kuwa na kiwango
tengemavu cha ubadilishaji wa fedha kitakachotokana na mwenendo wa soko la
fedha;
vii.
Kukua kwa
mikopo kwa sekta binafsi kwa kiwango cha asilimia 20 ya Pato la Taifa mwishoni
mwa Juni 2013 sambamba na jitihada za kudhibiti mfumuko wa bei;
viii.
Kuwa na akiba
ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na
huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne na nusu;
ix.
Kuimarisha
utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ili kupanua fursa za
kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo;
x.
Kuboresha
mazingira ya wafanya biashara wadogo na wakati;
xi.
Kulinda na
kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Sekta za huduma za jamii;
xii.
Kuimarisha
utawala bora na uwajibikaji; na
xiii.
Kujenga uwezo
wa nchi kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi na kifedha pamoja na kushiriki
kwa ufanisi katika ushirikiano kikanda na kimataifa.
Misingi ya Bajeti ya Serikali kwa Kipindi cha mwaka 2012/13
66.
Mheshimiwa Spika; ili kufikia malengo yaliyoainishwa
hapo juu, misingi ya Bajeti ya Serikali kwa kipindi cha mwaka 2012/13 ni hii
ifuatayo:
i.
Kuendelea
kuimarika kwa utengamavu wa viashiria vya uchumi jumla na maendeleo ya jamii;
ii.
Kuwepo kwa
nishati ya umeme wa uhakika na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia;
iii.
Kuimarika kwa
utekelezaji wa Sera za Fedha na Bajeti;
iv.
Kuendelea
kuimarika kwa mahusiano na Washirika wa Maendeleo;
v.
Kuendelea
kutekeleza sera ya ugatuaji wa madaraka kwa wananchi;
vi.
Kuendelea
kutekeleza maboresho katika sekta ya umma ikiwa ni pamoja na kuendelea
kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma;na
vii.
Kuendelea
kuboresha mazingira ya biashara pamoja na kuongezeka kwa tija na fursa za
uwekezaji.
Sera za Mapato
67.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea na azma yake ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa
kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo ya mapato yatokanayo na kodi na
yasiyotokana na kodi; na kupanua wigo wa makusanyo. Aidha, Serikali itaendelea
kuimarisha taratibu za kukusanya mapato pamoja na kupunguza misamaha ya kodi
ili kuweza kugharamia kwa kiwango kikubwa matumizi ya kawaida kwa kutumia
mapato ya ndani. Sera za mapato zitakazozingatiwa kwenye
Bajeti ya mwaka 2012/13 ni pamoja na;
i.
kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamiaji
wa mapato yasiyo ya kodi kwa kupitia upya mfumo wa utoaji
stakabadhi na leseni, pamoja na kuboresha viwango vya kubakiza maduhuli kwa
Wizara, Idara na Taasisi za Serikali;
ii.
kupanua wigo wa kodi kwa kuendelea kurasimisha sekta isiyo
rasmi ili iingie kwenye mfumo wa kodi;
iii.
kuendelea kufanya mapitio ya sheria za Wakala/Taasisi za
Umma zinazokusanya maduhuli ili ziweze kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa
Serikali;
iv. kuendelea
kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazotoa misamaha ya kodi kwa lengo
la kudhibiti na kupunguza misamaha hiyo;
v. Kupitia upya
mfumo wa ukusanyaji wa kodi ya majengo katika majiji, manispaa, miji, wilaya na
miji midogo ili kuuboresha zaidi;
vi. kufanya
mapitio ya vyanzo vya mapato na mfumo wa ukusanyaji katika Serikali za Mitaa
ili kuongeza mapato; na
vii. Kujenga
uwezo wa Wizara ya Fedha, Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo la
Petroli Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania, Wakala wa Ukaguzi wa Madini ili
kusimamia ukusanyaji wa mapato katika maeneo ya madini, gesi na petroli.
Hatua za Kuboresha Uzalishaji na
Huduma
68.
Mheshimiwa Spika, Serikali
imepokea mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waheshimiwa wabunge
kuhusu haja ya kuboresha mazingira ya uzalishaji katika sekta za Uvuvi,
Viwanda, Kilimo, Mifugo na Utalii. Hatua ambazo Serikali imepanga kuchukuwa ni
pamoja na:
i. Kupitia upya
vivutio kwa sekta ya viwanda vya ndani vinavyotumia malighafi za ndani vikiwemo
viwanda vya nguo na mafuta ya kula;
ii. Kutafuta
utaratibu mzuri wa kubainisha vipuri vya mashine na mitambo inayosamehewa kodi
ili kuondoa usumbufu wanaoupata waagizaji;
iii. Kupitia upya
viwango vya kodi katika sekta ya Kilimo na Uvuvi kwa lengo la kuviwianisha na
kupunguzwa;
iv. Kupitia upya
maudhui na viwango vya Tozo ya Kuendeleza Stadi (Skills Development Levy) na
Leseni ya Magari (Motor Vehicle Licence). Kwa kufanya hivyo, Serikali inalenga
katika kupanua wigo wa kodi, kuwapunguzia mzigo waajiri na kupanua ajira hapa
nchini. Aidha, mapitio ya Leseni za Magari yatazingatia kurejea madhumuni ya
kuanzishwa kwa leseni hiyo; na
v. Kufanya
mapitio ya Sheria ya VAT kwa lengo la kuibadili kwa kuzingatia uzoefu wa
kimataifa “Best Practice”.
69.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka za
Serikali za Mitaa zinahimizwa kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa
kuzingatia fursa zilizopo. Aidha, OWM – TAMISEMI kwa kushirikiana na Shirika la
Misaada na Utaalamu la Ujerumani – GIZ watakamilisha na kusambaza kwenye
Halmashauri mfumo wa kompyuta wa utunzaji kumbukumbu za mali na majengo
(Integrated Property Rating Information Management System - IPRIMS) ili
kuboresha ukusanyaji wa mapato hususan kodi ya majengo. Natoa rai kwa
Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali kuweka
msukumo utakaowezesha Halmashauri kukusanya kikamilifu kodi ya majengo pamoja
na mapato mengine ili kuziongezea uwezo wa kuhudumia wananchi na kuwaletea
maendeleo endelevu.
70.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
sera za mapato zilizoainishwa hapo juu, Serikali inalenga kukusanya mapato
ya ndani (bila kujumuisha Halmashauri) shilingi bilioni 8,714.7 sawa na
asilimia 18 ya Pato la Taifa. Kati ya kiwango hicho, mapato ya kodi shilingi
bilioni 7,080.1 na mapato yasiyo ya kodi shilingi bilioni 644.6. Mapato
yanayotokana na vyanzo vya Halmashauri shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia
0.7 ya Pato la Taifa.
Mikopo
ya Ndani
71.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea na utaratibu
wake wa kukopa katika soko la ndani la fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya
maendeleo na kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda
mfupi zinazoiva. Katika mwaka 2012/13, Serikali inakusudia kukopa kiasi cha
shilingi bilioni 1,632 kutoka soko la fedha la ndani. Kati ya kiasi hicho,
shilingi bilioni 483.9 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni kwa ajili ya
kugharimia miradi ya maendeleo na kiasi cha shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa
ajili ya kulipia hatifungani za Serikali na dhamana za Serikali za muda mfupi
zinazoiva. Kiwango hiki kimezingatia viashiria vya kiuchumi pamoja na
kuhakikisha kuwa Taasisi za Fedha zinaendelea kutoa mikopo kwa Sekta binafsi
ili kuchochea ukuaji wa uchumi.
Misaada
na Mikopo Mipya yenye Masharti Nafuu
72.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kushirikiana na
Washirika wa Maendeleo ili kuhakikisha Misaada na mikopo inapatikana kwa wakati
na kuchangia katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Katika bajeti ya mwaka
2012/13 serikali inatarajia kupata kiasi cha shilingi bilioni 3,156.7 kutokana
na misaada na mikopo yenye masharti nafuu. Kati ya fedha hizo, Misaada na
mikopo ya kibajeti ni shilingi bilioni 842, sawa na Dola za Marekani milioni
495. Misaada na mikopo kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha mifuko ya
kisekta inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2,314.2.
73.
Mheshimiwa Spika, pamoja na misukosuko ya kiuchumi
na majanga ya kiasili iliyozikumba nchi Wahisani, bado zimeendelea kutoa
misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwatambua
washirika wetu wa maendeleo ambao ni: Uingereza, Norway, Canada, Marekani,
Uholanzi, Ubelgiji, China, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Japani, Korea
ya Kusini, Denmark, Hispania, Sweden, Uswisi, India, Italia, Benki ya Dunia,
Benki ya Maendeleo ya Afrika, Umoja wa Ulaya, Global Funds, Shirika la Fedha la
Kimataifa (IMF), BADEA, Kuwait Fund, Nordic Fund, Opec Fund, Saudi Fund, na
Mashirika ya Umoja wa Mataifa. Tunawashukuru Sana.
Mikopo
ya nje yenye Masharti ya Kibiashara
74.
Mheshimiwa Spika, sera ya
Serikali ni kutafuta mikopo nafuu kutoka mashirika na nchi wahisani kwa ajili
ya kugharamia Bajeti yake ya maendeleo. Hata hivyo, kwa kuzingaita mahitaji
makubwa ya kuendeleza miradi ya miundombinu kwa mwaka 2012/13, Serikali
inatarajia kupata kutoka nje mikopo yenye masharti ya kibiashara kiasi cha
shilingi bilioni 1,254.1 sawa na Dola za Marekani milioni 749. Fedha hizi
zitatumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye
Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13 ikijumuisha mchango wa Serikali
(counterpart fund) katika ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam, mradi wa maji wa Ruvu chini na ujenzi wa barabara. Uamuzi wa kuendelea
kukopa kwa masharti nafuu na ya kibiashara unazingatia uhimilivu wa Deni la
Taifa uliopo.
Sera za Matumizi
75.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2012/13, sera za matumizi zitazingatia yafuatayo:
i. Matumizi
yataendelea kuzingatia mapato halisi yanayopatikana;
ii. Nakisi ya
bajeti haitazidi asilimia 5.5 ya Pato la Taifa, ikijumuisha ruzuku;
iii. Mafungu
yataendea kuzingatia viwango vya matumizi vitakavyoidhinishwa na Bunge;
iv. Maafisa
Masuuli wataendelea kuzingatia Sheria ya Fedha na ya Ununuzi wa Umma; na
v. Serikali
inaendelea kukusanya madeni yote kwa lengo la kuyahakiki na kuyapangia
utaratibu wa kuyalipa.
Matumizi ya Kawaida
76.
Mheshimiwa Spika, Sera za matumizi ya
kawaida kwa mwaka 2012/13 zinalenga pamoja na mambo mengine katika kugharamia
mishahara; madeni ya mikopo ya ndani na nje; uboreshaji wa huduma za kiuchumi
na maendeleo ya jamii; mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; mitihani ya shule
za msingi na sekondari; ununuzi na usambazaji wa dawa; mahitaji ya Tume ya
Kuratibu Mabadiliko ya Katiba; matengenezo ya mali ya Serikali; ununuzi wa
chakula cha hifadhi; mahitaji ya kawaida kwenye miradi iliyokamilika; pamoja na
kuendelea kulipa madai mbalimbali ya watumishi na wazabuni.
77.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana
na changamoto ya upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu, kilimo kisichokuwa na
tija na ukosefu wa ajira, Serikali imetenga fedha katika maeneo
yafuatayo: Shilingi bilioni 30 kwa ajili ya Benki ya Rasilimali; shilingi
bilioni 40 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo na hivyo kufikisha mtaji wa
shilingi bilioni 100. Aidha, shilingi bilioni 7.5 zimetengwa kwa ajili ya
kurejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, ambapo katika
awamu ya kwanza vijana 5,000 wanatarajiwa kujiunga. Vilevile, Serikali imetenga
jumla ya shilingi bilioni 70.7 katika maeneo mapya ikiwa ni Mikoa, Wilaya na
Halmashauri kugharamia matumizi ya kawaida na maendeleo.
Matumizi ya Maendeleo
78.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba
ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2011 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka
2012/13, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu Mhe. Stephen Masatu
Wasira, aliainisha miradi ya kitaifa ya kimkakati pamoja na miradi katika
maeneo muhimu ya ukuaji wa uchumi. Bajeti hii itazingatia vipaumbele hivyo:
a)
Miundombinu
i. umeme - mkazo
utawekwa katika upatikanaji wa umeme wa kuhakika kwa kuongeza uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji ambapo jumla shilingi bilioni 498.9 zimetengwa
kwa ajili hiyo. Aidha, Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa Bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa mkopo kutoka Benki ya Exim ya China wenye
thamani ya Dola za Marekani milioni 1,225.3 utakaosimamiwa na TPDC.
ii. usafirishaji
na uchukuzi – uimarishaji wa reli ya kati ikijumuisha ukarabati wa
injini na mabehewa ya treni. Kwa upande wa barabara, miradi inayopewa
kipaumbele ni pamoja na barabara zenye kufungua fursa za kiuchumi. Katika
usafiri wa anga na majini, miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi na
ukarabati wa viwanja vya ndege na uendelezaji wa gati ya Ziwa Tanganyika. Jumla
ya shilingi bilioni 1,382.9 zimetengwa katika eneo hili.
iii
maji safi na salama - kuongeza upatikanaji wa
maji safi na salama mijini na vijijini. Kiasi cha
shilingi bilioni 568.8 kimetengwa.
iv
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
– kuimarisha mawasiliano kwa kutumia TEHAMA ili
kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa
taarifa za masoko ya ndani na nje ya nchi; ukusanyaji wa mapato; huduma
za afya; elimu; huduma za kifedha; n.k. Jumla ya shilingi bilioni 4 zimetengwa
katika eneo hili.
b)
Kilimo, Uvuvi na Ufugaji
79.
Mheshimiwa Spika, kwa
kushirikiana na sekta binafsi, Serikali itawekeza katika
kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Wami, Ruvu, Kilombero na
Malagarasi pamoja na kuongeza tija na thamani, kubadilisha mfumo wa kilimo na
kukuza kilimo cha misitu. Hii ni pamoja na kuendeleza shughuli za ufugaji
na uvuvi ili ziwe na tija kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji; kwa kufanya
hivyo kutapunguza umaskini wa kipato.
80.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza uzalishaji wa mazao
ya chakula pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, Serikali itaimarisha utekelezaji wa
dhana ya Kilimo Kwanza kwa kuhakikisha kwamba nguzo zake zote zinaendelea
kuzingatiwa; kuhakikisha kwamba walengwa wanapata pembejeo kwa wakati; Maafisa
ugani kutakiwa kuwa na mashamba yao ya mfano (mashamba darasa) ili kuwaelimisha
wakulima kilimo cha kisasa; kuongeza msukumo kwenye kilimo cha umwagiliaji ili
wakulima waweze kufanya shughuli zao za kilimo katika misimu yote badala ya
kutegemea mvua;Kuimarisha masoko ya mazao kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko
ambayo imeshaanza shughuli zake; na Mikoa kutakiwa kuendelea kutenga
ardhi na vijiji kutakiwa kupima na kurasimisha ardhi kwa ajili ya wawekezaji wa
ndani na wa nje. Kiasi cha shilingi bilioni 192.2 kimetengwa katika
eneo hili.
c)
Maendeleo ya Viwanda
81.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini;
viwanda vinavyoongeza thamani ya madini; viwanda vikubwa vya saruji; na viwanda
vya eletroniki na TEHAMA pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na kutenga
maeneo maalum ya uwekezaji mijini na vijijini na kukuza ubia kati ya sekta ya
umma na sekta binafsi. Hatua hii inaenda sambamba na kuboresha na kuimarisha
viwanda vidogo vidogo nchini. Jumla ya shilingi bilioni 128.4 zimetengwa katika
eneo hili.
d)
Maendeleo ya Rasilimali Watu na Huduma za Jamii
82.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2012/13, Serikali imepanga kuboresha viwango vya elimu katika
ngazi zote hususan katika maeneo ya utafiti, ufundi stadi, afya; sayansi na
ujuzi maalum kuhusu madini, gesi, urani, chuma na mafuta; hatua hii inajumuisha
ukarabati wa maabara na upatikanaji wa vifaa vya maabara. Shilingi bilioni 84.1
zimetengwa katika eneo hili.
e)
Utalii
83.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kuboresha huduma zitolewazo katika eneo hili ikiwa ni pamoja na
kutangaza utalii na kuboresha mazingira ya kitalii na kutoa mafunzo ya utalii,
kuainisha maeneo mapya ya utalii na kuboresha vyuo vya utalii.
Huduma za Fedha
84.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kuimarisha huduma za kifedha hususan mifumo ya
kuweka akiba na kukopa kama vile SACCOS, VICOBA na benki za kijamii ili
kuwawezesha wananchi kupata mitaji kwa ajili ya biashara na uzalishaji. Kiasi
cha shilingi bilioni 2.6 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha mtaji wa Benki ya
Wanawake, Mradi wa SELF na Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi. Aidha, Wizara
ya Fedha itaendelea kusimamia maendeleo ya Taasisi za fedha zinazojihusisha na
utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali. Ili kufanikisha hili kitengo kilichopo cha
maendeleo ya sekta ya fedha kitahuishwa na kuwa idara kamili.
Usimamizi wa Fedha za Umma
85.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kutekeleza awamu ya nne ya Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa
Fedha za Umma na kuhakikisha kwamba Sheria ya Fedha za Umma na Sheria ya
Ununuzi wa Umma zinafuatwa kikamilifu ili kuongeza uwajibikaji katika matumizi
ya fedha za Umma. Maeneo yanayozingatiwa kwenye programu hiyo ni pamoja na:
kuendelea kuboresha Mtandao wa malipo (IFMS) ili kuimarisha udhibiti wa
matumizi ya fedha za Umma kwa Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
utoaji wa mafunzo ya ulipaji kwa mfumo wa malipo wa kibenki kwa watumishi wa
Ofisi za Bunge, Sekretarieti za Mikoa, Idara ya Ushirika, Ofisi ya Waziri Mkuu
-TAMISEMI na Ofisi za Hazina ndogo Mikoa yote. Aidha, Serikali itaendelea kutoa
mafunzo ya kuandaa hesabu kwa kutumia viwango vya uhasibu vya kimataifa ili
kuongeza uwazi katika matumizi ya fedha za Umma; kuijengea uwezo
Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha kanuni na
taratibu za matumizi ya fedha za umma zinazingatiwa ipasavyo; na kujenga uwezo
wa Serikali Kuu, Mikoa na Halmashauri katika eneo la uandaaji wa mipango na
bajeti, ukusanyaji wa mapato, usimamizi wa raslimali, uboreshaji wa mawasiliano
na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa bajeti.
86.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kuboresha utaratibu wa kupeleka fedha kwenye Halmashauri na kutoa
taarifa mapema kuhusu matumizi ya fedha zilizopelekwa. Aidha, fedha zote
zitakazovuka mwaka bila kutumika zitatolewa taarifa kwenye vikao vya Kamati za
Kudumu na Baraza la Madiwani ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa umma.
87.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2012/13, Serikali itaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi kwenye Wizara,
Idara, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri zote ili kuondoa
watumishi wasiostahili kwenye orodha ya malipo ya mishahara ya watumishi wa
Serikali. Aidha, mamlaka za ajira na maafisa masuuli wanaelekezwa kusitisha
malipo kwa watumishi walioacha au kuachishwa kazi, kustaafu, kufariki au likizo
bila malipo ili kuzuia upotevu wa fedha za umma.
88.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kutilia mkazo wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha za umma
katika Wizara, Taasisi, Wakala, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili
kuthibitisha endapo fedha zinazopangwa kukusanywa zinapatikana na pia fedha
zinazotumwa kutoka Hazina zinafika na kutekeleza shughuli zilizoidhinishwa.
Serikali itaboresha mifumo ya udhibiti na usimamizi wa fedha za umma
zinazokusanywa au kupelekwa kwenye Mikoa na Halmashauri nchini.
Usimamizi wa Mashirika ya Umma
89.
Mheshimiwa Spika, katika kukabliana na changamoto za
usimamizi wa Mashirika ya Umma, Serikali inaendelea kuimarisha Ofisi ya
Msajili wa Hazina kwa kufanya mapitio ya Sheria za Msajili wa Hazina ambazo ni
“Treasury Registrar Ordinance” ya mwaka 1958 na “Treasury Registrar Powers and
Functions” SURA 370 ya mwaka 2000 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 ili kuwa na
Sheria moja. Lengo la hatua hiyo ni kuimarisha ofisi kwa kuipa nguvu
zaidi za kisheria kuweza kusimamia ipasavyo utendaji wa Mashirika ya Umma
pamoja na Taasisi ili kuongeza tija.
Kukabiliana na Mfumuko wa Bei
90.
Mheshimiwa Spika, uchumi wetu unakabiliana na
changamoto nyingi ikiwemo mfumuko wa bei ambao kwa wastani umeshuka kutoka
asilimia 19.8 mwezi Desemba 2011 hadi asilimia 18.7 mwezi Aprili 2012.
Kichocheo kikubwa cha mfumuko wa bei ni kupanda kwa bei za umeme, mafuta na
vyakula hususan mchele na sukari. Kwa mfano kwa mwezi Aprili 2012, chakula
kimechangia asilimia 24.7 wakati umeme na mafuta vimechangia kwa asilimia 24.9.
Mfumuko wa bei ambao haujumuishi chakula na nishati bado uko kwenye tarakimu
moja ambayo ni asilimia 8.8. Hivyo, jitihada za Serikali zitaelekezwa katika
kukabiliana na kupanda kwa bei ya bidhaa hizo.
91.
Mheshimiwa Spika, hatua za haraka ambazo Serikali
itachukua ni pamoja na kutoa vibali vya uagizaji wa sukari na mchele kutoka nje
na kuendelea kuimarisha Hifadhi ya Chakula ya Taifa. Aidha, Serikali itawekeza
katika kilimo cha mpunga na miwa katika mabonde makuu ya Kilombero, Wami,
Kagera na Malagarasi pamoja na miradi ya kilimo cha umwagiliaji. Hatua nyingine
ni pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na
masoko; kuimarisha mfumo wa masoko kwenye maeneo yanayozalisha chakula kwa
wingi hususan mikoa ya nyanda za juu kusini na mipakani. Kwa upande wa nishati
ya umeme, Serikali itaendeleza vyanzo mbadala vya umeme kama vile umeme wa
gesi, nguvu za jua, upepo, miwa ili kupunguza matumizi ya mafuta kama chanzo
cha nishati.
Kupanua fursa za Ajira
92.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ajira hasa kwa vijana,
Serikali itaendelea kupanua huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuanzisha Benki
ya Kilimo na kuongeza mitaji kwa Benki za Rasilimali, Wanawake, Posta na Twiga
Bancorp. Hatua nyingine zitakazochukuliwa na kuchangia ongezeko la ajira ni
pamoja na kujenga miundombinu ya barabara, umeme, kilimo na mawasiliano. Aidha,
sekta binafsi itahamasishwa kutumia fursa zinazotolewa na Benki na Maendeleo ya
Afrika kupitia Dirisha la kuendeleza sekta binafsi. Kadhalika, Serikali
itaajiri watumishi 71,756 katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo na kada nyingine.
IV.
MABORESHO YA MFUMO WA KODI, ADA, TOZO NA HATUA NYINGINE ZA MAPATO:
93.
Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni,
Serikali imefanya maboresho katika mfumo wa kodi kwa nia ya kupanua wigo wa
kodi na kuongeza mapato ya ndani. Maboresho yaliyofanywa ni pamoja na
marekebisho ya sheria za kodi, kanuni na taratibu za usimamiaji wa kodi. Aidha
hatua hizi zimechangia katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo
ya kodi. Hata hivyo kuna changamoto katika kuhuisha mapato ya ndani ili
kupunguza utegemezi wa bajeti hatua kwa hatua. Kwa
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
kuzingatia hali hiyo Serikali itaendelea kuchukua hatua zenye kuboresha sera za kodi na usimamiaji wa mapato.
94.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza mafanikio
yaliyopatikana kwenye mfumo wa kodi, napendekeza kufanya maboresho katika
sheria mbalimbali za kodi kama ifuatavyo:-
a)
Sheria ya Kodi
ya Ongezeko la Thamani, SURA 148;
b)
Sheria ya Kodi
ya Mapato, SURA 332;
c)
Sheria ya
Ushuru wa Bidhaa, SURA 147;
d)
Sheria ya
Ushuru wa Mauzo Nje, SURA 196;
e)
Sheria ya Kodi
ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
f)
Sheria ya
Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
g)
Sheria ya
Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
h)
Misamaha ya
Kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali
(GNs);
i)
Marekebisho
mengine katika baadhi ya sheria za kodi na sheria za Usimamizi wa Fedha; na
j)
Marekebisho ya
Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea.
k)
Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004;
A. Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148
95. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani, SURA 148 kama ifuatavyo: -
(i)
Kuanzisha
kiwango kipya (VAT Rate) cha asilimia 10 cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa
baadhi ya watu, taasisi na mashirika yanayopata unafuu wa kodi
hiyo
(special
relief). Kwa mantiki hiyo, wale waliokuwa hawalipi kodi hiyo kuanzia sasa
watalipa asilimia 10. Hatua hii itazihusu Kampuni binafsi, watu binafsi na
Kampuni zitakazopewa vyeti vya Kituo cha Uwekezaji Tanzania isipokuwa zile
zenye vyeti hivyo kwa sasa. Aidha, itahusu pia Mashirika yasiyo ya Kiserikali
isipokuwa yale yaliyopewa msamaha wa kodi pale yanapotoa huduma ya
chakula, dawa baridi na vifaa kama vile sabuni ambavyo vinatolewa msaada kwenye
vituo mahsusi vya kulelea watoto yatima na shule;
(ii)
Kurekebisha
kifungu cha 19 cha Jedwali la Pili la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili
kuongeza Mashine za Elektroniki za kutoa stakabadhi za kodi (Electronic Fiscal
Devices - “EFDs”) katika orodha ya vifaa vinavyopata msamaha wa kodi hiyo.
Lengo ni kuwawezesha walipa kodi kupata vifaa hivi kwa gharama nafuu na
kuhamasisha matumizi yake kwa kuwa ni muhimu katika kutoa stakabadhi za mauzo
ya bidhaa na huduma;
(iii)
Kusamehe Kodi
ya Ongezeko la Thamani kwa Vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya gesi
iliyoshindiliwa na gesi ya mabomba (Compressed Natural Gas and Piped Natural
Gas). Msamaha wa kodi unatolewa ili kuhamasisha matumizi ya gesi katika magari,
kupikia, nyumbani, taasisi na viwandani. Aidha, Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC) litawajibika kuhakiki vifaa hivyo ili kuhakikisha kwamba vitatumika
kujenga miundo mbinu ya gesi.
96.
Mheshimiwa Spika,
Mitambo na vifaa vya kujenga miundombinu ya gesi asili vinavyoombewa msamaha wa
kodi ni kama ifuatavyo:-
- CNG vehicles conversion kits – vifaa vinavyoongezewa kwenye magari yaweze kutembea kwa kutumia nishati ya gesi asili;
- High pressure vessels (CNG and LPG cylinders) – mitungi maalumu ya kutunzia gesi asili iliyoshindiliwa na gesi ya LPG;
- Natural Gas Compression plants equipments – vifaa kwa ajili ya mitambo ya kushindilia gesi asili;
- Natural gas pipes (Transportation and Distribution pipes) – mabomba maalum ya kusafirishia na kusambazia gesi asili;
- CNG storage cascades – mitungi maalum ya pamoja ya kusafirishia na kuhifadhia gesi asili iliyoshindiliwa;
- CNG transportation trailers - magari na matela ya kusafirishia gesi asili iliyoshindiliwa;
- Natural gas metering equipments – mita za kupimia kiasi cha gesi asili;
- Pipeline fittings and valves – vifaa vya kuunganishia mabomba na kuruhusu/kuzuia gesi kupita;
- CNG Refueling/filling equipment – vifaa vya kujazia gesi asili kwenye magari;
- PNG/CNG accessories – vifaa vidogo vidogo vinavyotumika katika ujenzi wa mabomba ya gesi asili na katika mitambo ya kushindilia gesi asili;
- Gas Receiving Unit – vifaa vya kupokelea gesi ya mabomba;
- Condensate Stabilizer – vifaa vya mifumo ya kuimarisha uhifadhi wa condensate;
- Flare Gas System – vifaa kwa ajili ya mifumo ya kuunguza gesi kwa ajili ya usalama;
- Air & Nitrogen System – vifaa vya mifumo ya hewa na ya Nitrogen;
- Condensate Tanks and Loading Facility – matanki ya kuhifadhia condensate na vifaa vya kupakilia;
- System piping on piperack – mifumo ya kubeba mabomba ya gesi asili;
- Instrumentation – vifaa vya umeme na udhibiti kwenye mifumo ya gesi asili.
- Majiko yaliyotengenezwa mahsusi kwa ajili ya matumizi ya gesi pekee.
Hatua hizi katika Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa pamoja
zitaongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 22,565.1
B.
Sheria ya Kodi ya Mapato, SURA 332
97. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya
Mapato, SURA 332 kama ifuatavyo: -
- Kuweka kiwango cha chini cha mapato ghafi ya wafanyabiashara wadogo cha shilingi 3,000,000 kisichotozwa kodi na kurekebisha matabaka (bands) ya walipa kodi. Lengo la hatua hii ni kulinda mapato halisi ya Serikali na kuhakikisha kwamba wenye mapato ya chini ya kiwango cha kutozwa kodi cha shilingi 3,000,000 hawatozwi kodi chini ya mfumo wa kukadiria kodi Walipa kodi wadogo “Presumptive Scheme” kama ilivyo kwenye mapato yatokanayo na ajira. Hivi sasa Wafanyabiashara wenye kipato hicho wanatozwa Sh. 35,000.
Viwango vya sasa na
vinavyopendekezwa ni kama ifuatavyo: -
Viwango vya sasa
Thamani ya Mauzo
|
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
|
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
|
||
(i)
|
Kwa mauzo yasiyozidi Shs.
3,000,000/=
|
Shs.
35,000/=
|
1.1% ya mauzo
|
|
(ii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs.
3,000,000/= na yasiyozidi Shs. 7,000,000/=
|
Shs.
95,000/=
|
Shs. 33,000/= + 1.3% ya mauzo
yanayozidi Shs. 3,000,000/=
|
|
(iii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs.
7,000,000/= na yasiyozidi Shs. 14,000,000/=
|
Shs.
291,000/=
|
Shs. 85,000/= + 2.5% ya mauzo
yanayozidi 7,000,000/=
|
|
(iv)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs.
14,000,000/= na yasiyozidi Shs. 20,000,000/=
|
Shs.
520,000/=
|
Shs. 260,000/= + 3.3% ya mauzo
yanayozidi Shs. 14,000,000/=
|
|
Viwango vinavyopendekezwa
|
||||
Thamani ya Mauzo
|
Kodi kwa wasiokuwa na kumbukumbu za mauzo
|
Kodi kwa wenye kumbukumbu za mauzo
|
||
(i)
|
Kwa mauzo yasiyozidi Shs.
3,000,000/=
|
Asilimia
sifuri (0%)
|
Asilimia sifuri (0%)
|
|
(ii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs
3,000,000/= na yasiyozidi Shs 7,500,000/=
|
Shs.
100,000/=
|
2% ya mauzo yanayozidi
Shs 3,000,000/=
|
|
(iii)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs
7,500,000/= na yasiyozidi Shs 11,500,000/=
|
Shs.
212,000/=
|
Shs. 90,000/= plus 2.5% ya mauzo
yanayozidi Shs 7,500,000/=
|
|
(iv)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs
11,500,000/= na yasiyozidi Shs 16,000,000/=
|
Shs.
364,000/=
|
Shs. 190,000/= + 3.0% ya mauzo
yanayozidi Shs 11,500,000/=
|
|
(v)
|
Kwa mauzo yanayozidi Shs
16,000,000/= na yasiyozidi Shs 20,000,000/=
|
Shs.
575,000/=
|
Shs. 325,000/= + 3.5% ya mauzo
yanayozidi Shs 16,000,000/=
|
|
- Kutoza Kodi ya Zuio ya asilimia 10 kwenye mapato yatokanayo na riba inayotolewa na mabenki kwa wafanyabiashara ambao si wakaazi (non-residents). Lengo ni kuweka usawa kwa walipa kodi wote.
- Kufanya marekebisho ya kifungu cha 54 (2) cha sheria ya kodi ya mapato ili kufuta msamaha wa kodi ya mapato kwa makampuni yenye hisa zipatazo asilimia 25 au zaidi. Lengo la marekebisho haya ni kuleta usawa kwa walipa kodi wanapopata gawio.
- Kuanzisha kodi itokanayo na uuzaji wa raslimali ya uwekezaji (capital gains tax) kwenye uuzaji wa hisa za kampuni za ndani unaofanywa na Kampuni mama ya nje ya nchi.
- Kuongeza kima cha chini cha kutozwa kodi (threshold) kwenye mapato ya ajira kutoka shilingi 135,000 hadi 170,000. Hatua hii itaongeza kipato kwa mfanyakazi.
- Kutoa msamaha wa Kodi ya Mapato kwa soko la Hisa la Dar es Salaam (Dar es salaam Stock Exchange). Lengo ni kulifanya soko hilo kukua.
- Kusamehe Kodi ya Mapato (kwa wenye leseni) yatokanayo na michezo ya kubahatisha iliyokwishalipiwa kodi chini ya sheria ya kodi ya michezo ya kubahatisha, SURA 41. Lengo la hatua hii ni kuepusha wenye leseni za biashara ya michezo ya kubahatisha kulipa kodi mara mbili.
- Kusamehe Kodi ya Zuio kwenye riba ya mikopo inayotozwa na mabenki ya nje kwa wawekezaji wanaowekeza kwenye sekta na shughuli muhimu katika mkakati wa kukuza uchumi (Strategic Investors). Lengo la hatua hii ni kutoa unafuu kwa wawekezaji hao wanapopata mikopo kutoka kwenye mabenki ya nje ya nchi na hivyo kuhamasisha uwekezaji hapa nchini.
Hatua hizi za Kodi ya Mapato zitaongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 105,672.3
C.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147
98. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru
wa Bidhaa, SURA 147 kama ifuatavyo:-
- Kufuta Ushuru wa bidhaa uliokuwa unatozwa kwenye mafuta mazito ya kuendeshea mitambo. Hivi sasa mafuta hayo yanatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 40 kwa lita. Lengo la hatua hii ni kupunguza gharama za uzalishaji katika viwanda hapa nchini. Aidha, hatua hii itaongeza uzalishaji na kuleta ushindani sawa kwa wenye viwanda katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kuwa nchi nyingine hivi sasa hazitozi ushuru kwenye bidhaa hiyo.
- Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha wasanii kudurufiwa kazi zao za sanaa na kukosa maslahi kwa kazi wanazofanya. Ili kutatua tatizo hili, Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato itaanza kurasimisha biashara ya bidhaa za muziki na filamu kwa nia ya kuhakikisha kwamba uasili wake unatambulika na hivyo kuzuia vitendo vya kudurufu kazi za sanaa (piracy of artists work) hali ambayo inadumaza ukuaji wa sanaa na vipaji hapa nchini. Aidha, Mamlaka ya Mapato itaweka stampu kwenye bidhaa hizo ili uuzaji wa kazi hizo uwe rasmi na kuwawezesha wasanii kupata kipato stahili kutokana na kazi zao. Vilevile hatua hii itaiingizia serikali mapato.
Kwa kuwa yanahitajika maandalizi ya kutosha ikiwa ni
pamoja na kurekebisha sheria na kanuni mbalimbali, utekelezaji wa hatua hii
utaanza rasmi tarehe 1 Januari, 2013.
- Kufuta msamaha wa Ushuru wa Bidhaa kwa magari kwa wote waliokuwa wananufaika na msamaha huo isipokuwa kwa miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye mkataba, mashirika ya dini, Balozi, Ofisi za Balozi, Wanabalozi na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and Diplomatic Missions). Aidha haitahusu Kampuni za Madini zenye mikataba yenye kutoa misamaha.
- Ili kulinda viwanda vya hapa nchini vinavyotengeneza maji ya matunda (juisi) dhidi ya ushindani usio haki wa bidhaa hiyo kutoka nje, maji ya matunda kutoka nje yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 83 kwa lita ambapo yanayozalishwa hapa nchini yatatozwa ushuru wa bidhaa wa shilingi 8 tu kwa lita.;
- Kurejea msamaha wa ushuru wa mafuta ya petroli (fuel levy) uliotolewa mwaka 2011/12 kwenye mafuta yanayotumika kuendesha meli, na vifaa vingine vinavyotumika katika utafiti wa mafuta na gesi ili usomeke kama Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwenye mafuta ya Petroli.
- Napendekeza kufanya marekebisho kwenye Ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye pombe, vinywaji baridi, sigara, na mvinyo kama ifuatavyo: -
a. Vinywaji baridi kutoka shilingi 69
kwa lita hadi shilingi 83 kwa lita ikiwa ni nyongeza ya shilingi 14;
b. Mvinyo uliotengenezwa kwa Zabibu
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango kinachozidi asilimia 75 kutoka shilingi
420 kwa lita hadi shilingi 145 kwa lita, ikiwa ni punguzo la shilingi 275;
c. Mvinyo uliotengenezwa kwa zabibu
inayozalishwa nje ya nchi kwa kiwango kinachozidi asilimia 25, kutoka shilingi
1,345 kwa lita hadi shilingi 1,614 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi
269;
d. Vinywaji
vikali, kutoka shilingi 1,993 kwa lita hadi shilingi 2,392 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 399.
e. Bia inayotengenezwa na nafaka ya
hapa nchini na ambayo haijaoteshwa, kutoka shilingi 248 kwa lita hadi shilingi
310 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 62;
f. Bia nyingine zote, kutoka shilingi
420 kwa lita hadi shilingi 525 kwa lita, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 105 sawa
na shilingi 52.5 kwa chupa yenye ujazo wa nusu lita;
Marekebisho ya viwango vya Ushuru wa bidhaa kwenye
sigara ni kama ifuatavyo: -
a)
Sigara zisizo na kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi
6,820 hadi shilingi 8,210 kwa sigara elfu moja. Hii ni sawa na nyongeza ya shilingi 1,390 kwa sigara
elfu moja au shilingi 1.4 kwa sigara moja;
b)
Sigara zenye kichungi na zinazotengenezwa kutokana na tumbaku
inayozalishwa hapa nchini kwa kiwango cha angalau asilimia 75, kutoka shilingi
16,114 hadi shilingi 19,410 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 3,296
au shilingi 3.3 kwa sigara moja;
c)
Sigara nyingine zenye sifa tofauti na (a) na (b) kutoka shilingi
29,264 hadi shilingi 35,117 kwa sigara elfu moja, ikiwa ni nyongeza ya shilingi 5,853
sawa na shilingi 5.8 kwa sigara moja;
d)
Tumbaku ambayo iko tayari kutengeneza sigara (cut filler) kutoka
shilingi 14,780 hadi shilingi 17,736 kwa kilo, ikiwa ni nyongeza ya
shilingi 2,956 kwa kilo; na,
e)
Ushuru wa “Cigar”
unabaki kuwa asilimia 30.
- Kutoza Ushuru wa bidhaa kwenye Gesi asilia inayotumika viwandani kwa kiwango cha Shilingi 0.35 kwa kila futi ya ujazo (Shs 0.35 per cubic feet);
- Kuongeza Ushuru wa bidhaa kwenye muda wa maongezi (airtime) kwenye simu za mkononi kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 12. Lengo la hatua hii ni kuwianisha ushuru wa bidhaa unaotozwa kwa huduma hii katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa wakati huu ambapo tupo kwenye soko la pamoja.
Hatua
hizi katika Ushuru wa Bidhaa kwa pamoja zinatarajiwa kuongeza mapato ya
Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 144,054.9
D.
Sheria ya Ushuru wa Mauzo Nje, Sura 196;
99.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kuongeza kiwango cha
Ushuru wa mauzo nje (export levy) kwenye bidhaa za ngozi ghafi zinazosafirishwa
kwenda nje ya nchi kutoka asilimia 40 za sasa au Shilingi 400 kwa kilo moja
hadi asilimia 90 au Shilingi 900 kwa kilo moja kutegemea kiwango kipi ni
kikubwa. Lengo la hatua hii ni kuhamasisha usindikaji wa ngozi hapa
nchini na kuongeza thamani ya bidhaa za ngozi. Aidha hatua hii itachangia
katika kukuza ajira viwandani na kuongeza mapato ya Serikali.
Hatua
hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 26,431.8
E. Sheria ya Kodi
ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming Act), SURA, 41;
100. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya Kubahatisha (Gaming
Act), SURA 41; kama ifuatavyo:-
i.
Kuongeza tozo
la Gaming Tax kwa casino kutoka asilimia 13 ya mapato ghafi ya mchezo wa
kubahatisha (Gross Gaming Revenue) hadi asilimia 15;
ii.
Kutoza tozo
kwenye michezo ya Utabiri wa matokeo ya michezo (Sports Betting) kwa asilimia 6
ya “total stakes”;
iii.
Kutoza tozo la
Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 43 kwenye michezo ya “SMS Lotteries”;
iv.
Kutoza tozo la
Gaming Tax kwa kiwango cha asilimia 15 kwa michezo ya Internet Casino.
v.
Kuweka
kipengele katika Sheria ya Kodi ya Michezo ya kubahatisha kinachotamka kwamba
“gaming tax shall be conclusive tax”.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza mapato ya serikali kwa
kiasi cha shilingi milioni 6,360.
F. Sheria ya
Usajili na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124;
101. Mheshimiwa
Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Usajili
na Uhamishaji wa Magari, SURA, 124 kwa kuanzisha utaratibu wa kumiliki usajili
wa namba za magari zenye utambulisho wa taarifa za mtu binafsi kwenye gari lake
kwa ada ya shilingi 5,000,000 kwa miaka mitatu.
Hatua
hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 50
G. Sheria ya
Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365;
102. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika Sheria ya Ushuru wa Viwanja vya Ndege, SURA, 365 kwa
kuongeza tozo ya huduma za viwanja vya ndege (Airport Service Charges) kutoka
kiwango cha sasa cha Dola za Kimarekani 30 hadi Dola 40 kwa safari za nje na
kutoka Shilingi za Tanzania 5,000 hadi Shilingi 10,000 kwa safari za ndani.
Hatua
hii inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 11,597.7
H. Misamaha ya
kodi ya magari kupitia sheria za kodi na matangazo ya Serikali (GNs)
103. Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya
marekebisho kwenye sheria husika za kodi na matangazo ya Serikali yanayotoa
msamaha wa kodi kwenye magari kwa walengwa mbalimbali ili kuweka ukomo wa umri
wa miaka nane (8) kwa magari hayo badala ya miaka 10. Aidha, magari yenye umri
wa zaidi ya miaka nane (8) yatatozwa Ushuru wa bidhaa wa asilimia 20. Lengo la
hatua hii ni kupunguza wimbi la uagizaji wa magari chakavu na kulinda
mazingira.
I.
Marekebisho mengine katika baadhi ya Sheria za Kodi na sheria za Usimamizi wa
Fedha
104. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho mengine madogo madogo yasiyo ya kisera katika Sheria
mbalimbali za kodi ili ziwe sanjari na azma ya kurahisisha utekelezaji wake.
105.
Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho katika sheria ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki,
SURA 231 ili kwanza, kuweka kinga dhidi ya mali zinazomilikiwa na Benki
ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ikiwemo nyumba, akiba, fedha na akaunti za
benki dhidi ya mashauri ya kisheria, maamuzi ya kimahakama na utaifishaji. Pili,
kuipa hadhi ya mdai benki hii kama ilivyo kwa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa
(IMF), Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuiwezesha kupewa
upendeleo endapo yatatokea matatizo yoyote katika soko la fedha. Tatu,
kumpa mamlaka Waziri wa Fedha kutekeleza maamuzi ya Baraza la uongozi
(Governing Board) la EADB kwa kurekebisha Jedwali la Sheria hii kupitia Tangazo
la Serikali na baadaye kuwasilisha taarifa Bungeni. Nne, kutoa
tafsiri ya mali za benki ili kutoa ufafanuzi kwamba mali za benki ni pamoja na
nyumba za benki, akiba za fedha zilizokasimiwa kwa EADB kwa ajili ya utendaji
wake.
J. Marekebisho ya
Ada na Tozo Mbalimbali za Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea
106. Mheshimiwa Spika, napendekeza
kufanya marekebisho ya viwango vya ada na tozo mbali mbali zinazotozwa na
Wizara, Mikoa na Idara zinazojitegemea ili kuvihuisha kulingana na hali halisi
ya ukuaji wa uchumi.
K. Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ya mwaka 2004
107. Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa
Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya Kikao cha maandalizi ya Bajeti
(Pre-Budget Consultations of EAC Ministers for Finance) mnamo tarehe 18 Mei
2012 jijini Kampala, Uganda. Kikao hicho kilipendekeza marekebisho ya viwango
vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha (EAC-Common External Tariff “CET”) na Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kwa
mwaka wa fedha wa 2012/13. Mapendekezo hayo yanalenga katika kuboresha
Sekta za Viwanda, Usafirishaji, Afya, Nishati, Mifugo, Mawasiliano na Habari.
108.
Mheshimiwa Spika, maeneo yanayopendekezwa kufanyiwa
marekebisho kwenye viwango vya Ushuru wa Pamoja wa Forodha ni: -
i. Kutoza ushuru wa asilimia sifuri
(0%) badala ya asilimia 35 kwenye ngano inayotambuliwa katika HS Code
1001.90.20 na HS Code 1001.90.90 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Lengo la hatua
hii ni kupunguza gharama za uingizaji wa bidhaa hii nchini kwa vile uzalishaji
wa ndani bado ni wa chini kuweza kutosheleza mahitaji.
ii. Kuongeza Ushuru wa Forodha kwenye
galvanized wire kutoka asilimia sifuri (0%) hadi asilimia 10 inayotambuliwa
katika HS Code 7217.20.00. Hatua hii inalenga katika kuwianisha viwango vya
utozaji wa Ushuru wa Forodha kwa vile bidhaa hii inatengenezwa kutokana na hot
rolled steel wire rods zinazotambuliwa katika HS Code 7213.20.00 ambayo
inatozwa ushuru wa asilimia 10.
iii. Kutenganishwa kwa bidhaa
zinazotambulika katika HS Code 2106.90.91 ili kutenganisha virutubisho vya
chakula na madini (food supplements and mineral premix) vinavyotumika katika
kutengeneza chakula cha watoto wachanga na kuzitoza Ushuru wa Forodha wa
asilimia sifuri (0%). Hatua hii inalenga katika kuwezesha watoto wachanga na
wagonjwa kuweza kupata vyakula vyenye virutubisho kwa bei nafuu na kuimarisha
afya zao.
iv. Kupunguza Ushuru wa Forodha kutoka
asilimia 25 hadi asilimia sifuri kwenye ving’amuzi (set top boxes)
vinavyotambuliwa katika HS Code 8528.71.00 ili kuwezesha mabadiliko ya kutoka
katika teknolojia ya analogi na kwenda katika teknolojia ya digitali. Hatua hii
inatekeleza makubaliano ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwamba
ifikapo Desemba 2015 ziwe zimetoka kwenye mfumo wa utangazaji wa analogi kwenda
digitali.
v. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye
umeme (HS Code 2716.00.00) kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri (0%). Hatua
hii inalenga katika kupunguza gharama ya umeme unaonunuliwa kutoka nje ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji katika
nchi hizo.
vi. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye
glasi za ndani (inner glass) za chupa za chai (thermos) zinozotambuliwa katika
HS Code 7020.00.90 kutoka asilimia 25 hadi asilimia sifuri ili kutoa unafuu na
kuchochea ukuaji wa viwanda vya kuunganisha chupa za chai katika nchi za
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa bidhaa hiyo haipatikani katika Jumuiya.
vii. Kutenganisha programu (software)
inayotambulika katika HS Code 8523.80.00 ili kutoza Ushuru wa Forodha wa
asilimia sifuri (0%). Lengo ni kuhamasisha ukuaji wa Sekta ya Mawasiliano na
hivyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
viii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
(duty remission) kwenye malighafi ya kutengeneza sabuni (Palm Sterini, RBD)
inayotambuliwa katika HS Code 1511.90.40 kwa kipindi cha mwaka moja. Hatua hii
inalenga katika kuvipa unafuu viwanda vidogo vya kutengeneza sabuni hapa nchini
na kuviwezesha kumudu ushindani katika bidhaa hiyo inapoingizwa kutoka nje.
ix. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
(duty remission) kwa malighafi ya kutengeneza sabuni inayojulikana kama LABSA
inayotambuliwa katika HS Code 3402.11.00; HS Code 3402.12.00 na HS Code
3402.19.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja. Hatua hii inalenga katika kuimarisha
uzalishaji na kukuza viwanda vidogo vya sabuni nchini.
x. Kupunguza Ushuru wa Forodha kwenye
bidhaa inayojulikana kama cathodes inayotambuliwa katika HS Code 7403.11.00
kutoka asilimia 10 hadi sifuri (0%). Hivi sasa bidhaa hii inatozwa ushuru wa
asilimia 10 ambapo shaba iliyotengenezwa kwa ukamilifu (refined alloys/refined
copper) hutozwa ushuru wa asilimia (0%), ambapo ni kinyume na matakwa ya sheria
ya ushuru wa forodha ya jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004. Lengo la
hatua hii ni kuwianisha ushuru wa malighafi inayotumika kuzalisha bidhaa hii
ili iendane na kanuni/taratibu za kutoza ushuru zinazozingatia viwango vya
usindikaji.
xi. Kuendelea kutoza Ushuru wa Forodha
wa asilimia 25 badala ya asilimia 35 kwenye saruji inayotambuliwa katika HS
Code 2523.90.00 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
xii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
(duty remission) kwa wazalishaji wanaotumia mafuta ya kutengeneza vilainishi
(castor oil and its fraction) inayotambuliwa katika HS Code 1515.30.00 Hatua
hii imezingatia kwamba bidhaa hii ni mali ghafi inayotumika katika kutengeneza
vilainishi;
xiii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
kwenye vyuma vinavyowekwa kwenye kingo za barabara vijulikanavyo kama road
guard rails kwa kutenganisha HS Code 7308.90.90. Lengo ni kutoa unafuu katika
ujenzi wa miundombinu ya barabara. Aidha, hatua hii inazingatia kwamba bidhaa
hii haizalishwi kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya soko la Jumuiya ya Afrika
Mashariki;
109.
Mheshimiwa Spika, Mawaziri wa Fedha wa Nchi Wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walifanya marekebisho kwenye Sheria ya Forodha
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC-Customs Management Act, 2004) kama
ifuatavyo:-
i. Kufanya marekebisho katika Kifungu
30(b) cha Sehemu B ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ili kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye mitambo (machinery) na
vipuri vyake vinavyotumika kwenye uchimbaji wa madini. Msamaha huu
hautahusisha vipuri vya magari vitakavyoagizwa na makampuni yanayojihusisha na
uchimbaji wa madini.
ii. Kufanya marekebisho katika aya ya 22
(a) ya Jedwali la Tano la Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
kuongeza “refrigerated trailers” katika bidhaa zinazopata msamaha wa Ushuru wa
Forodha. Hatua hii inalenga katika kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha kwenye
magari ya trela yenye majokofu ili kuimarisha biashara ya usambazaji bidhaa
kama vile nyama, maziwa n.k.
iii. Kutoa msamaha wa Ushuru wa Forodha
kwenye malighafi zinazotumika katika kutengeneza vifaa vya kufanyia uchunguzi
wa magonjwa (medical diagnostic kits) kwa kuwa vifaa hivyo hutozwa asilimia
sifuri (0%) vinapoagizwa kutoka nje. Aidha, lengo pia ni kuhamasisha uzalishaji
wa bidhaa hiyo katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
iv. Kufanya marekebisho katika Jedwali
la Tano, B kwenye aya ya 15 ili kuongeza vifaa vinavyotumika katika ufugaji na
kurina asali na kuvipa msamaha wa ushuru wa forodha vinapoagizwa nje na
wafugaji wa nyuki. Lengo ni kuhamasisha na kuchochea ukuaji wa sekta ya ufugaji
wa nyuki.
v. Kuendelea kutoa msamaha wa Ushuru wa
Forodha kwenye migahawa ya Majeshi ya Ulinzi kwa kipindi cha mwaka mmoja.
vi. Kufanya marekebisho katika Sheria ya
Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 ili kutoa msamaha wa
Ushuru wa Forodha (duty remission) kwa wazalishaji wa vyakula vinavyotengenezwa
mahsusi kwa lishe ya watoto wenye utapia mlo na watu wanaoishi na virusi vya
ukimwi. Hatua hii inalenga katika kuwawezesha kupata vyakula hivyo kwa gharama
nafuu na kuboresha afya zao.
110.
Mheshimiwa Spika, Marekebisho mengine ninayotarajia
kufanya kwenye Ushuru wa Forodha ni kama ifuatavyo: -
i.
Kufuta msamaha
wa Ushuru wa Forodha kwa magari yenye ujazo wa cc 3000. Hatua hii haitahusu
miradi inayotekelezwa kwa misaada ya wafadhili yenye msamaha wa kodi kwenye
mikataba, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa (Diplomats and
Diplomatic missions).
ii.
Kupunguza
msamaha wa kodi uliokuwa unatolewa kwenye bidhaa zinazotambulika kama “deemed
capital goods” kutoka asilimia 100 hadi asilimia 90. Kwa mantiki
hiyo, mwekezaji atatakiwa kulipa asilimia 10 ya kodi zote zinazotozwa kwenye
bidhaa husika.
Hatua
hizi kwa pamoja zinatarajiwa kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha
shilingi milioni 12,805
Mheshimiwa Spika, hatua zote za
mapato kwa ujumla zimezingatia azma ya Serikali ya kukuza uchumi na kuongeza
mapato ili hatimaye kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani. Aidha,
ili kutekeleza azma hiyo, hatua za mapato zinalenga katika kupunguza misamaha
ya kodi hatua kwa hatua ili kufikia kiwango cha asilimia 1 ya Pato la Taifa
kama ilivyo katika nchi nyingine Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
L.
Tarehe ya Kuanza Kutekeleza Hatua Mpya za Kodi
111. Mheshimiwa Spika, hatua hizi za
kodi zinazopendekezwa zitaanza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2012, isipokuwa pale
ilipoelezwa vinginevyo.
V. SURA YA BAJETI KWA MWAKA 2012/13
112. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia sera za
uchumi pamoja na misingi na sera za
bajeti, Serikali inatarajia kukusanya shilingi bilioni 15,119.6. Kati ya mapato
hayo, Serikali inalenga
kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 8,714.8
sawa na
asilimia 18 ya Pato la Taifa. Aidha, mapato kutokana na vyanzo vya Halmashauri
ni shilingi bilioni 362.2 sawa na asilimia 0.7 ya Pato la Taifa.
113. Mheshimiwa
Spika, Washirika wa
Maendeleo wanatarajiwa kuendelea kutusaidia mwakani kwa kutupatia misaada na
mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 3,156.7. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 842.5 ni misaada na mikopo ya kibajeti na shilingi
bilioni 2,314.2 ni mikopo na misaada kwa ajili ya miradi ya
maendeleo, ikijumuisha Basket Funds na fedha za Millenium Challenge Account
(MCA - T).
114. Mheshimiwa
Spika, Serikali inategemea kukopa kiasi cha
shilingi bilioni 2,886.1 kutoka vyanzo vya ndani na nje kuziba pengo la mapato.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 1,148.1 ni kwa ajili ya kulipia
hatifungani na dhamana za Serikali za muda mfupi zinazoiva, shilingi bilioni
483.9 ambayo ni asilimia moja ya Pato la Taifa na shilingi bilioni 1,254.1 ni
mikopo yenye masharti ya kibiashara.
115. Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa
matumizi, Serikali imepanga kutumia jumla ya shilingi bilioni 15,119.6 katika
mwaka 2012/13 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Jumla ya
shilingi bilioni 10,591.8 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida
ikijumuisha shilingi bilioni 3,781.1 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa
Serikali, Taasisi na Wakala za Serikali na shilingi bilioni 2,745.1 kwa ajili
ya Mfuko Mkuu wa Serikali. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 4,527.8 zimetengwa
kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 2,213.6
kitagharamiwa kwa fedha za ndani na shilingi bilioni 2,314.2 kitagharamiwa kwa
fedha za nje (misaada na mikopo ya miradi ya maendeleo ikijumuisha miradi ya
MCA (T) na basket fund).
116. Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia
mfumo wa bajeti kama ulivyoelezwa hapo juu, sura ya bajeti kwa mwaka 2012/13
inakuwa kama ifuatavyo:-
Mapato
|
Shilingi Milioni
|
|||
A.
|
Mapato ya Ndani
|
8,714,671
|
||
(i) Mapato ya Kodi
(TRA)
|
8,070,088
|
|||
(ii) Mapato yasiyo ya Kodi
|
644,583
|
|||
B.
|
Mapato ya Halmashauri
|
362,206
|
||
C.
|
Mikopo na Misaada ya Kibajeti
|
842,487
|
||
D.
|
Mikopo na Misaada ya Miradi ya
Maendeleo ikijumuisha MCA (T)
|
2,314,231
|
||
E.
|
Mikopo ya Ndani
|
1,631,957
|
||
F.
|
Mikopo yenye Masharti ya
Kibiashara
|
1,254,092
|
||
JUMLA YA MAPATO YOTE
|
15,119,644
|
|||
Matumizi
|
||||
G.
|
Matumizi ya Kawaida
|
10,591,805
|
||
(i) Deni la
Taifa
|
2,745,056
|
|||
(ii) Mishahara
|
3,781,100
|
|||
(iii) Matumizi Mengineyo
|
4,065,649
|
|||
Wizara
3,311,399
|
||||
Mikoa
49,701
|
||||
Halmashauri 704,549
|
||||
H.
|
Matumizi ya Maendeleo
|
4,527,839
|
||
(i) Fedha za Ndani
|
2,213,608
|
|||
(ii) Fedha za Nje
|
2,314,231
|
|||
JUMLA YA MATUMIZI YOTE
|
15,119,644
|
|||
117.
Mheshimiwa
Spika, mambo yaliyozingatiwa wakati wa mgao wa fedha kwa bajeti ya
mwaka 2012/13 ni pamoja na yafuatayo:-
i.
Kuweka mafungu yote katika kiwango cha
mgao wa fedha kinacholingana na matarajio ya matumizi ya mafungu husika kwa
mwaka 2011/12;
ii.
Kuyatengea fedha matumizi
yasiyoepukika kama vile posho za kisheria, “ration allowance”, nk.
iii.
Maeneo mapya ya utawala;
iv.
Fedha zinazotolewa kwa wizara zenye
utaratibu wa kubakiza (retention);
v.
Maeneo ya vipaumbele (strategic na
non-strategic).
118. Mheshimiwa
Spika, bajeti ninayoiwasilisha ina uwiano wa asilimia 70 kwa matumizi
ya kawaida na asilimia 30 kwa matumizi ya maendeleo. Viwango hivyo
vya uwiano vimezingatia ukweli kwamba makisio ya matumizi ya maendeleo kwa
fedha za ndani ya Shilingi 1,871.5 bilioni na makisio ya matumizi ya maendeleo
kwa fedha za nje ya Shilingi 3,054.1 bilioni yenye jumla ya Shilingi 4,925.6
kwa mwaka 2011/12 hayatafikiwa. Hivyo, inatarajiwa kwamba hali halisi ya
matumizi ya maendeleo itakuwa Shilingi 2,983 bilioni ambayo ni karibu ya
asilimia 22. Kwa kipindi kilichoishia Aprili, 2012 matumizi ya maendeleo kwa
fedha za ndani yalifikia 1,201.6 bilioni na matumizi ya maendeleo kwa fedha za
nje ni shilingi 1,450.4 bilioni. Sababu za kutofikiwa kwa malengo hayo ya
matumizi nimezieleza hapo awali ikiwa ni pamoja na kutopatikana kwa fedha za
mikopo ya kibiashara na kuchelewa kwa fedha za misaada na mikopo ya
miradi ya maendeleo kutoka kwa wahisani. Aidha, uwiano huo umezingatia
maeneo niliyoyataja hapo juu ambayo ni matumizi muhimu.
VI.
HITIMISHO
119. Mheshimiwa Spika, Serikali
kupitia bajeti hii imejipanga kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2012/13
ambao unaelekeza uwekezaji wa rasilimali za Taifa kwenye maeneo machache
ya kipaumbele kwa lengo la kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi na
kupunguza umaskini. Serikali itaendelea kuhamasisha sekta binafsi kwa kuwekeza
zaidi katika maeneo ya kipaumbele. Aidha, kila mwananchi anapaswa kushiriki
kikamilifu katika kutumia fursa zinazojitokeza kwa kutoa huduma na kuzalisha
mali ili kujiongezea kipato.
120.
Mheshimiwa Spika, kufanikiwa kwa Bajeti ya Mwaka
2012/13 kunahitaji nidhamu ya hali ya juu kwa kila Wizara, Idara, Mikoa,
Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato na matumizi
ya fedha za umma. Matumizi yasiyokuwa na tija na ambayo si muhimu ni vyema
yakaepukwa. Sekta binafsi ina uwezo mkubwa wa kuchangia katika uchumi. Hivyo,
ni muhimu kila Wizara, Idara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa fursa
kwa sekta binafsi ili waweze kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa Taifa
letu.
121.
Mheshimiwa Spika, Mkutano wa Bunge la Bajeti
mwaka huu unafanyika miezi michache kabla ya zoezi muhimu la Sensa ya Watu
na Makazi itakayofanyika tarehe 26 Agosti 2012. Kauli mbiu ya sensa ya mwaka
huu ni ‘‘Sensa kwa Maendeleo Jiandae Kuhesabiwa’’. Napenda kutoa wito
kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi wengine katika ngazi zote kuhamasisha
wananchi kushiriki katika zoezi hili ambalo matokeo yake yatawezesha kupata
takwimu muhimu zitakazowezesha Serikali kupanga mipango kwa ajili ya maendeleo
ya wananchi kwa usahihi.
122.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia
nafasi hii kuwashukuru wapiga kura wangu wote wa Jimbo la Kalenga kwa
kunichagua kuwa Mbunge wao na kwa ushirikiano wanaonipatia. Napenda kuwaahidi
kuwa nitaendelea kushirikiana nanyi kuliletea maendeleo Jimbo letu la Kalenga.
Mwisho namshukuru mke wangu mpendwa pamoja na familia kwa kuwa msaada kwangu
katika kutekeleza majukumu haya mapya.
123.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment