Monday, October 17, 2011

BAISKELI YAPATA WADHAMINI ZAIDI

Afisa Udhamini wa  Vodacom Tanzania ,Ibrahim Kaude(kulia) na Meneja uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania ,Matina Nkurlu wakimwangalia Maneja wa kinywaji cha Malta Guinnes Maurice Njowoka akisoma mkataba mara baada ya kusaini makubaliano ya kuwa mdhamini mwenza wa Mashindano ya Baiskeli ya Vodacom Mwanza openi cycle Challenge  kupitia kinywaji cha Malta Guinnes,mbio hizo zitafanyika  October 22 kuanzia shinyanga mpaka jijini Mwanza.
serengeti breweries kuwa wadhamini wenza wa mashindano ya baiskeli ya vodacom mwanza open cycle challenge.

Serengeti Breweries kuwa mdhamini mwenza 'Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge'.
Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Limited SBL kupitia kinywaji chao cha Malta Guinness imejitosa kudhamini mbio za baiskeli zijulikanazo kama "Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge" zitakazofanyika Oktoba 22 mwaka huu jijini Mwanza.

Kwa mwaka huu mashindano hayo yatakuwa maalum kwani yatashirikisha mbio za kilomita 196 kwa wanaume, 80 kwa wanawake ambapo kwa upande wa walemavu ni Kilometa 15 kwa walemavu wanaume na Kilomita 10 kwa walemavu wanawake.

Akizungumzia udhamini huo Meneja wa Kinywaji cha Malta Guinness Maurice Njowoka amesema wamedhamini mbio hizo za "Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge" kwa kiasi cha shilingi Milioni 7/- ili kuongeza chachu na ari ya mbio hizo. Akifafanua zaidi Njowoka amesema kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania wameamua kudhamini mbio hizo zilizofikia hadhi ya kimataifa ili washiriki wanufaike na mbio hizo wakati wakitumia fursa hiyo kujiweka fiti kiafya.

"Mbio za "Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge" zitakazofanyika jijini Mwanza mwaka huu sasa zimefikia hadhi ya kimataifa kutokana na makundi ya watu wanaohudhuria. Kutokana na hilo SBL kupitia Malta Guinness tumeona tuwe mmoja ya  wadhamini  wa mbio hizo," amesema Njowoka.

Kwa upande wake Matina Nkurlu ambaye ni Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao wa Vodacom Tanzania ameishukuru Kampuni ya bia ya SBL kupitia kinywaji chake cha Malta Guinness kwa kuwa mmoja ya wadhamini wa mbio hizo zinazotarajia kushirikisha waendesha baiskeli zaidi ya 500. Vilevile Nkurlu amebainisha kwamba lengo la kampuni yake kuandaa na kudhamini mashindano hayo ni kuyafanya mashindano hayo kuwa ya kimataifa na hatimaye kutoa mwakilishi atakayepeperusha vema bendera ya Tanzania katika medani za kimataifa siku za usoni.

"Kupitia  uandaaji wa mchezo  wenye thamani ya 50m na huu wa wadau wetu Serengeti Breweries ni matarajio yetu mmoja ya washiriki kutokana na michuano hii  atatwaa ubingwa kwenye michuano ya kimataifa ya baiskeli kama ile ya 'Tour de France' inayofanyika kila mwaka nchini Ufaransa.

Mbali na hayo Nkurlu amewahamasisha washiriki kujitokeza na kujiandikisha kwa wingi ili wajipatie zawadi kwenye mbio hizo zitakazoanzia mkoani  Shinyanga na kumalizikia jijini Mwanza Oktoba 22 mwaka huu.
Amezitaja zawadi hizo kwa washiriki wa mbio za kilometa 150  mshindi wa kwanza atajipatia shilingi 1,500,000, wa pili kiasi cha 1,000,000, wa tatu 700,000, ambapo mshindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atajipatia shilingi 500,000 kila mmoja.

Kwa upande wa mbio za mita 80 kwa wanawake mshindi wa kwanza pia atajipatia zawadi ya shilingi milioni 1,100,000, wa pili 800,000, mshindi wa tatu 600,000, wakati washindi wa nne hadi wa kumi kila mmoja atazawadia kiasi cha shilingi 350,000 kila mmoja. Aidha Meneja huyo ameeleza kwamba kwa upande wa mbio za kilometa 15 ambazo zitawashirikisha watu wenye ulemavu alisema washindi wa kwanza wawili kila mmoja atajipatia jumla ya shilingi 500,000.

Kwa washindi wa pili wawili nao watajishindia kiasi cha shilingi 250,000 kila mmoja, washindi wa tatu wawili kila mmoja atapewa kiasi cha 150,000 kila mmoja wakati washindi wa nne wane  hadi wa kumi watajipatia kitita cha 100,000 kila mmoja.Na watakaoshika nafasi ya 11 hadi ya 20 katika mbio hizo  watazawadiwa kiasi cha shilingi 70,000 Vodacom Tanzania pia imekuwa  ikidhamini michezo mbalimbali kama vile Soka, Riadha, kuogelea, mashindano ya boti, mashindano ya Mbuzi, Vodacom Miss Tanzania, Tenisi na mingine mingi ili kuhakikisha kwamba taifa linafanya vizuri katika tasnia nzima ya michezo.

No comments:

Post a Comment