Friday, May 4, 2012

MKUTANO MKUU WA MWAKA WA BARRICK GOLD MINE WAMZUIA MWANAHARAKATI KUTOKA TANZANIA KUHUDHURIA


Mwanaharakati wa Haki za binadamu na mwanasheria wa masuala ya Maliasili Mr. Amani Mustafa Mhinda, ambaye pia ni Mkurugenzi wa asasi ya kijamii ya HAKIMADINI,inayoshughulika na haki za binadamu katika maeneo ya machimbo ya madini akiwa anawahutubia wanaharakati nje ya jengo ampako mkutano wa barrick ulifanyika
Mkutano wa mwaka huu wa Barrick Gold Mine uliofanyika Toronto Nchini Canada May 3, 2012, ulimzuia Mwanaharakati wa Haki za binadamu na mwanasheria wa masuala ya Maliasili Mr. Amani Mustafa Mhinda, ambaye pia ni Mkurugenzi wa asasi ya kijamii ya HAKIMADINI,inayoshughulika na haki za binadamu katika maeneo ya machimbo ya madini.

Mhinda alikuwa amedhamiria kueleza wahudhuriaji wa Mkutano huo kuhusu umuhimu wa kujenga uwezo wa wachimbaji wadogo na jamii zinazoishi katika maeneo ya machimbo, ili ziweze kunufaika na rasilimali ya madini ya Tanzania, pamoja na kulinda na kutetea haki zao, ambayo pia ni agenda kuu ya HAKIMADINI yenye makao yake makuu mjini Arusha.



Pamoja na kuwa na ajenda hiyo, Barrick Gold na uongozi wake walimzuia kuingia katika eneo la mkutano huo.

Akinukuliwa na gazeti moja la kitaifa la Canada liitwalo The Canadian, Mhinda alieleza uhalali wake wa kuhudhuria mkutano huu huku akinukuu matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu yanayofanywa na makampuni ya uchimbaji

“Kama shirika lisilo la kiserikali la kitanzania na wananchi wa Tanzania, tunataka kuona mauaji na uvunjwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na makampuni ya uchimbaji madini ya Canada yanamalizwa. Niko hapa kumwakilisha watanzania wengi ambao ni wahanga wa mgodi huu pamoja na Mama Otaigo, aliyefariki mwezi wa nne kwa kunywa maji yenye sumu yaliyopo karibu na Mgodi wa North Mara”. Amani alisema

Mwanaharakati huyo pamoja na wanaharakati wengine wa masuala ya haki za binadamu walinyimwa kuzungumza kuhusu matendo ya kinyanyasaji yanayofanyika kwenye maeneo ya machimbo ya madini nchini Tanzania katika mkutano Mkuu wa Mwaka wa Barrick Gold mine.

Hatua hiyo ya kampuni ya Barrick Gold Mine kuwazuia wanaharakati wa Tanzania na kuwaruhusu wenzao wa nchi kama Papua New Guines na Chile kuliushangaza umati wa waalikwa kwenye mkutano huo.

Mhinda alishutumu hatua iliyochukuliwa na Barick Gold ya kumzuia kuingia katika mkutano huo kama “juhudi za wazi za kuficha uvunjwaji wa haki za binadamu unaofanywa na makampuni ya uchimbaji na wawekezaji wengine kwa jamii za kitanzania".

Pamoja na kufungiwa kuingia katika mkutano huo, Amani na wanaharakati wengine walipata nafasi ya kuelezea habari zao kwa maelfu ya watu waliokusanyika nje ya eneo la Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Barrick kwa ajili ya kupinga unyanyasaji unaofanywa na kampuni ya Barrick Gold ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya uchimbaji dhahabu duniani, iliyoanzishwa na kusimamiwa na Peter Munk.

Miongoni mwa wajumbe wa bodi ya kampuni hiyo ni pamoja na Waziri mkuu wa zamani wa Canada. Barick hupata fedha za serikali na misaada ya kidiplomasia. Makao makuu ya barrack yapo Toronto, Canada, wakati Africa Barrick, ni kampuni ya Uingereza ambayo humilikiwa kwa 70% na Barrick Gold

No comments:

Post a Comment