Saturday, May 5, 2012

SIMBA YATWAA UBINGWA SOKA BARA


WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC ya jijini Dar es Salaam,  leo wametawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa soka Tanzania Bara.
Simba, ambayo iko kambini Zenji kujifua kwa mpambano wake na watani wa jadi Yanga kesho,  imetwaa taji hilo lililokuwa likishikiliwa na mtani wao huyo, kutokana na ushindi wa mabao 2-1 ilioupata Mtibwa Sugar dhidi ya Azam FC leo.Azam FC na Mtibwa Sugar, ziliamriwa kurudiana  baada ya mechi yao ya awali kuvunjwa na mwamuzi Rashid Msangi dakika ya 88, matokeo yakiwa 1-1, kabla ya Kamati ya Ligi kuja kuipa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu, uamuzi uliokuja kukatiwa rufaa na klabu ya African Lyon.
Kutokana na rufaa hiyo, Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi, iliamua mchezo huo urudiwe jana kwenye kiwanja huru, kutokana na waamuzi kubainika kuharibu pambano hilo.Katika mchezo wa leo, Mtibwa ikishangiliwa kwa nguvu na mashabiki wanaosadikika kuwa ni wa Simba na Yanga, ilijipatia bao la kwanza dakika ya 25, likifungwa na bao Awadh kwa shuti kali la nje ya 18, akipokea mpira wa kona ya Juma Abdul. Matokeo yaliyodumu hadi mapumziko.Kipindi cha pili, Juma Abdul aliiandikia Mtibwa bao la pili kwa shuti kali kwa mpira wa faulo, kabla ya John Boko kuipatia Azam FC bao la kufutia machozi, dakika ya 69.Dakika ya 89, kipa wa Mtibwa Deo Munishi, alilimwa kadi ya pili ya njano na mwamuzi Oden Mbaga, kwa kupoteza muda na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Sharrif.Kwa matokeo hayo, Mtibwa imefikisha pointi 39 huku Azam ikibaki na pointi 53, zote zikiwa zimeshuka dimbani mara 25, zikibakiza mechi moja mkononi.Hivyo hata Azam ikishinda mchezo wake uliobakia itafikisha pointi 56, huku Simba iliyoko kileleni ikiwa na pointi 59 na mchezo mmoja mkononi dhidi ya watani wao Yanga wenye pointi 49.Pazia la Ligi Kuu bara, litafungwa kesho kwa timu zote 14 kushuka dimbani katika mikoa mbalimbali.Katika mbio za kusaka mfungaji bora, Boko amezidi kujihakikishia kiatu cha dhahabu, baada ya kufikisha mabao 18 huku akifuatiwa kwa mbali na Hamis Kiiza wa Yanga mwenye mabao 11.

No comments:

Post a Comment