Watanzania wengi bado
hatujaweza kutambua uwezo mkubwa tuliokuwa nao katika kuchangia maendeleo yetu.
Inaeleweka kwamba kumekuwa na kilio kikubwa kuhusu michango ya kila siku katika
sekta ya elimu. Hatahivyo mengi ya malalamiko haya yanatokana zaidi na wasiwasi
wa matumizi ya michango husika. Michango hii ikielekezwa mahala stahiki na
kuhusisha wachangiaji juu ya matumizi yake ina uwezo mkubwa sana wa kubadilisha
maisha ya watoto wetu walioko mashuleni.Tatizo sio UWEZO, tatizo hasa ni NIA.
Watanzania kwa kiasi
kikubwa tumekuwa na utamaduni wa kuchangia zaidi shughuli zinazoshahabiana na
anasa kuliko kuchangia maendeleo. Kwa wenzetu wakenya kuchangia watoto wa
majirani kwenda shule ni sehemu ya utamaduni uliojikita. Mathalani kwa mkoa wa
Dar es Salaam ambapo kuna watanzania zaidi ya milioni nne watu 100,000
huudhuria sherehe za harusi kwa mwezi kiwango cha chini cha uchangiaji kawaida
ni Tshs 60,000. Kama hii ndiyo hali inamaanisha kuwa kwa mwaka sisi wakazi wa
Dar es Salaam tunatumia kiasi cha shillingi 72,000,000,000,000 kiasi ambacho
kingeweza kupeleka watoto 720,000 kwa gharama ya Shillingi 100,000 kwa mwaka.
Kwahiyo tungetoa asilimia kumi tu ya matumizi yetu kwenye harusi tungepeleka
watoto 72,000 shule kila mwaka!!!Labda tutaulumu mfumo wetu wa ujamaa kwa
kutuzoesha kwamba tungeweza kupata huduma zote toka serikalini. Serikali ikawa
ndio baba ndio mama na hivyo hata wajibu wa kimsingi kama kupata elimu ya
msingi tukaiachia serikali. Umiliki wetu wa jambo hili la msingi na lazima
ukapotea kwa utaratibu huo.
Ni rahisi kusema kuwa
serikali inakusanya kodi kwahiyo ifanye kila kitu lakini ni sawa na kuomba
rafiki yako amtunze mwanao wakati ukilipia gharama za matunzo hayo. Ni dhahiri
bado utahitaji kuingia gharama za kuhakikisha mwanao anapata matunzo
yanayokidhi mahitaji na ndipo hapo kila mara utakapomtembelea mwanao utajikuta
ukiongeza kagharama kidogo ka kununua pipi, kubadili nepi, kubadili maziwa na
vitu vingine vidogo vidogo ambavyo huwa haviachi kuibuka. Bila shaka wote
tukichulia elimu kwa uzito tunaouchukulia watoto wetu wa kuzaa tunaweza kupiga
hatua.Natoa wito kwa kila mmoja wetu kutafakari nafasi yake katika maendeleo ya
elimu nchini. Tunaweza kuendelea kukaa kimya au kuchukua hatua sasa.
Nwakaribisha vile vile kuendeleza mjadala kupitia ukurasa wa faceboo @Educate
the Children of Tanzania na kupitia twitter @shujaawakarne.Mwandishi wa makala
haya ni Katibu Mtendaji wa asasi ya EDUCATE THE CHILDREN; asasi ya kitanzania
inayojihusisha na kuchochea upatikanaji wa elimu bora kwa watoto wa kitanzania
na kwa namna ya pekee watoto wanaotoka kwenye familia duni.
No comments:
Post a Comment