Wednesday, November 23, 2011

WASANII TUMIENI KISWAHILI SANIFU KATIKA KAZI ZENU - BASATA

Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Habari kutoka BASATA, Godfrey Mngereza akisisitiza jambo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA. Kulia ni Mchamba kutoka UKUTA.Mtendaji kutoka Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) Mchamba A. Mchamba (Kulia) akiongea na Wadau wa Sanaa juu ya Ushairi na Usanifu wa Lugha ya Kiswahili Katika Kazi za Sanaa kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Utafiti, Mafunzo na Habari, BASATA Godfrey Mngereza.Mkongwe wa Muziki wa Dansi na Mwanaharakati wa Sanaa

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka Wasanii kutumia Kiswahili sanifu katika kazi zao, kama hakuna sababu ya msingi ya kufanya vinginevyo hasa ya kisanii.

Akizungumza ofisini kwake wiki hii muda mfupi kabla ya Programu maalum ya kuwapa elimu Wasanii juu ya Ushairi na Utumizi wa Lugha Sanifu Katika Sanaa, Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego alisema kuwa, ni muhimu kwa Wasanii kutumia lugha sanifu katika kazi zao kutokana na ukweli kuwa, wanasikilizwa na watu wengi na ni kioo cha jamii.

“Wasanii wana mchango mkubwa katika kukuza Kiswahili. Wanatakiwa kutumia lugha fasaha na iliyosanifiwa ingawa hili haliwabani pale wanapotakiwa kuvaa uhusika katika kazi wanazozifanya hasa uigaji wa lafudhi na utumizi wa lugha kulingana na maeneo au mazingira” alisema Materego.

Aliongeza kuwa, kuna baadhi ya mazingira kitaaluma ndani ya Sanaa yanawaruhusu Wasanii kutumia lugha vinginevyo lakini hili ni pale tu wanapotakiwa kuvaa uhusika na si inavyofanywa na baaadhi ya Wasanii kupotosha lugha makusudi.

“Kuna suala la uhusika na ufikishaji ujumbe katika kazi za Sanaa, hili linampa fursa Msanii kuitumia lugha kulingana na haja na mazingira. Msanii akiwa katika hali hiyo kwa kweli ni katika kutekeleza majukumu yake” alisisitiza Materego.

Awali akiongea na Wadau wa Sanaa kwenye programu hiyo, Mtendaji kutoka Usanifu wa Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA), Mchamba A. Mchamba alisema kuwa, kumekuwa na upotoshaji wa lugha miongoni mwa Wasanii hali ambayo imekuwa ikivuruga Lugha hiyo.

Alitoa wito kwa Wasanii na Waandishi wa habari kuwa mabalozi wema katika kukisambaza Kiswahili sanifu kutokana na ukweli kuwa, wanaaminiwa, kusikilizwa na kusomwa sana na watu wa kada mbalimbali.

“Wasanii na Waandishi wanaaminiwa, kusikilizwa na kusomwa sana. Kila wanachoongea kinachukuliwa na jamii kama kilivyo. Ni vema wakawa mstari wa mbele kutumia lugha sanifu kwani itawapa heshima na kuipa thamani kazi yao” aliongeza.

No comments:

Post a Comment