Monday, December 19, 2011

Uchumi wa Taifa hatarini: Mfumuko wa Bei ni tishio kwa Serikali, Wafanyabishara na Wananchi

Mfumuko wa Bei umezidi kuongezeka kama taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu inavyoonesha kwamba, wakati mfumuko wa bei mwezi Julai mwaka huu (Bajeti ya mwaka wa Fedha 2011/2012 ilipokuwa inaanza) ulikuwa asilimia 13, umefikia asilimia 19.2 mwezi Novemba. 
Hii maana yake ni kwamba, Bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni 2011, imepunguza uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6. 
Hii ni sawa na shilingi 780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi Minne tu ya utekelezaji wa wake. Kutokana na kasi ya ukuaji wa Mfumuko wa Bei ni dhahiri kwamba, itakapofika mwisho wa mwaka wa Bajeti Serikali itakuwa imepoteza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kununua bidhaa na huduma kwa zaidi ya robo ya Bajeti yake.
Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kwani Mfumuko wa Bei za vyakula umekua kwa kasi kikubwa mno. Ofisi ya Takwimu imeonesha kuwa wakati mfumuko wa Bei za vyakula ulikuwa asilimia 14.8 mwezi Julai, umefikia asilimia 24.7 mwezi Novemba 2011. 
Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo katika ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa shilingi 10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa shilingi 12,500. 
Bei za vyakula zimeongezeka kwa kiwango hiki ilhali kipato cha mwananchi aghalabu kipo pale pale. Mwathirika mkubwa ni mwananchi wa kawaida wa kijijini ambaye mapato yake ni kidogo na hivyo sehemu kubwa huyatumia kununua chakula.
Ukiangalia kwa undani utakuta mfumuko wa bei wa bidhaa kama mchele, sukari, nyama na samaki umekua maradufu. Bei ya mchele imekua kwa asilimia 50, sukari asilimia 50, nyama asilimia 30 na Samaki kwa takribani asilimia 40. Bidhaa hizi zote ni muhimu sana kwa afya ya binadaamu na hasa watoto kwa upande wa vyakula vya protini. Tusipokuwa makini na kupata majibu sahihi ya tatizo la mfumuko wa bei za vyakula,wananchi wengi na hasa watoto watapata utapiamlo na Taifa kuingia gharama kubwa katika kuwapatia huduma ya afya.
Kwa upande wa bidhaa zisizo za vyakula, mfumuko wa bei wa mafuta ya taa na gesi asilia unapaa kwa kasi kama moto wa nyikani. Wakati mafuta ya taa yamepanda bei kwa asilimia 71 katika ya mwezi Novemba mwaka 2010 na mwezi Novemba 2011, bei ya gesi asilia imepanda kwa asilimia 35. 
Madhara ya hali hii ni makubwa mno maana wananchi watakimbilia kwenye matumizi ya mkaa na kuni, hata hivyo bei za mkaa zenyewe zimepanda kwa asilimia 24. Kwa hali hii, na kutokana na ukweli kwamba wananchi wengi wa Tanzania wapo kwenye mpaka wa umasikini na daraja la kati chini, juhudi za muongo mzima za kupunguza umasikini zitafutwa ndani ya mwaka mmoja tu.
Mfumuko wa Bei unasukuma Watanzania wengi zaidi kwenye dimbwi la umasikini, unapunguza uwezo wa Serikali kutoa huduma za jamii kupitia Bajeti na hata kutimiza mipango ya miradi ya maendeleo kama miundombinu ya barabara, umeme, bomba la gesi, madaraja nk. Mkakati mahususi unatakiwa kubadili hali hii. Hatua zifuatazo zinapendekezwa ili kuuhami uchumi na kupunguza upandaji wa kasi wa gharama za maisha.
1. Kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kuweka mbinu za kukuza uchumi wa vijijini ni njia mojawapo endelevu ya kupunguza mfumuko wa Bei hapa nchini. Serikali sasa iache maneno matupu kuhusu sekta ya uchumi vijijini kwa kuelekeza nguvu nyingi huko. 
Serikali iruhusu na ivutie kwa kasi na kutoa vivutio kwa wazalishaji binafsi wa Sukari na mpunga katika mabonde makubwa. Waziri wa Kilimo na Maafisa wake watoke Ofisini na kuhimiza uzalishaji mashambani, fedha zielekezwe kujenga miundombinu ya barabara vijijini.
Vyakula vilivyolundikana mikoa ya Mbeya, Iringa na Rukwa ambapo Serikali iliahidi kununua na kutotimiza ahadi yake vinunuliwe mara moja na kusambazwa mikoa yenye shida ya chakula kama Mwanza, Mara, Kagera na mikoa ya Kaskazini. Chakula kukuta msimu mwingine katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ni kashfa kubwa kwa Serikali na inaonesha Serikali isivyokuwa makini na maisha ya wananchi.
Wakati huu ambapo tunaweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula, Serikali inunue chakula cha kutosha na hasa mchele na sukari kutoka nje na kukisambaza kwenye soko ili kupunguza upungufu wa bidhaa (scarcity) katika masoko.
Mfumo uliotumika kununua Sukari tani laki moja hivi karibuni usitumike tena kwani ulizaa rushwa ya hatari na ufisadi ambao haujaripotiwa kwenye kutoa vibali. Wizara ya Kilimo iruhusu wauzaji kutoka nje walete sukari nchini moja kwa moja na kununuliwa na Bodi ya Sukari kisha kuiuza kwa wauzaji wa Jumla. Mfumo wa kutoa vibali umeonesha kutokuwa na tija na kwa kweli kunufaisha maafisa wachache wa Wizara ya Kilimo na Bodi ya Sukari.
2. Kitengenezwe kiwanda cha kutengeneza gesi ya matumizi nyumbani (LPG extraction plant) kwa haraka ili kupunguza bei ya gesi, kuepuka kuagiza gesi kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni na kutengeneza ajira hapa nchini. Kupanda kwa bei ya gesi asilia kunatokana na kwamba Tanzania inaagiza gesi hii yote kutoka nje ilhali malighafi ya kutengeneza gesi ipo hapa Tanzania na kwa kweli huchomwa moto (flared). 
Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini liingie ubia na kampuni Binafsi ili kuwekeza katika kiwanda cha kuzalisha gesi hatimaye kushusha bei na hivyo kuwezesha wananchi wengi zaidi kutumia gesi kwa matumizi ya kupikia n.k, hivyo kutunza mazingira.
3. Ushuru wote unaokusanywa kwenye Mafuta ya Taa upelekwe Wakala wa Nishati Vijijini ili kufidia kupanda kwa bei ya mafuta ya Taa. Mfumuko wa Bei katika bidhaa ya mafuta ya taa unatokana na uamuzi wa kuwianisha bei ya mafuta ya taa na diseli ili kuondoa tatizo la uchakachuaji wa mafuta. 
Tatizo limeondoka (au hatulisikii tena) lakini wananchi wanaumia sana. Uamuzi sahihi wa kisera ni kupanua huduma za umeme vijijini kwa kuipa fedha zinazotokana na ushuru wa mafuta ya taa Wakala wa Umeme Vijijini. 
Usambazaji wa Umeme Vijijini utaongeza shughuli za kiuchumi vijijini, kukuza uchumi wa vijijini, kuongeza mapato ya wananchi kwa kuongeza thamani za mazao yao na hivyo kupunguza athari za mfumuko wa bei.
4. Sera ya Matumizi ya Serikali iangaliwe upya kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi yasiyo ya lazima, na kuelekeza fedha nyingi zaidi katika uwekezaji umma (public investments). Matumizi Mengineyo ya Serikali yanaongeza fedha kwenye mzunguko ama kwa kulipa watu wachache stahili mbalimbali kama posho n.k au kwa kununua bidhaa na huduma bila mpango, na hivyo kusukuma bei kuwa juu kinyume na uhalisia wa soko. Tafiti za mfumuko wa Bei Tanzania zinaonyesha kwamba sera za fedha na zile za matumizi (monetary and fiscal policy) zina nafasi kubwa katika kukuza mfumuko wa bei. 
Hivi sasa nakisi ya Bajeti inayopelekea Serikali kukopa kwa kwa kiwango kubwa inapandisha gharama za viwanda kukopa mitaji ya muda mfupi na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji na kasha bei za bidhaa. Wizara ya Fedha ambayo mpaka sasa imekaa kama imeishiwa namna ya kufanya, inapaswa kuamka na kutoa maelekezo mapya kwa Wizara, Idara na Wakala za Serikali kuhusu namna ya kubana matumizi na kuziba mianya yote ya kukwepa kodi.
Hitimisho
Serikali imeonesha udhaifu mkubwa sana katika kusimamia uchumi katika nusu ya kwanza ya Bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo pia ni Bajeti ya kwanza ya kipindi cha pili cha Serikali ya awamu wa Nne.
 Kuna hatari ya dhahiri kwamba ifikapo mwezi Januari 2012 tutakuwa tumerejea mfumuko wa Bei wa kiwango cha mwaka 1992 (21.9%). Tusipochukua hatua za haraka tutafikia na hata kuzidi mfumuko wa Bei kiwango cha juu kabisa ambacho kilifikiwa mwaka 1994 (33%) na hivyo viwanda kushindwa kukopa kwenye Mabenki kwa mahitaji yao ya haraka ya mitaji ya muda mfupi, wazalishaji wadogo kushindwa kulipa mikopo yao kwenye Taasisi za fedha na hivyo kufunga uzalishaji, Shirika la Umeme kushindwa kabisa kulipa gharama za mafuta ya kuendesha mitambo na kipato cha mwananchi kutomudu gharama za za kila siku. Uchumi utadorora kabisa. Taifa litakuwa hatarini.
Wizara ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Kilimo na Chakula iamke kuhami uchumi dhidi ya adui namba moja, Mfumuko wa Bei. Huu sio wakati wa kupiga porojo, viongozi wafanye kazi zao, Wananchi wajitume.
Inabidi sasa turejee kauli mbiu za miaka 50 iliyopita za Uhuru ni Kazi. Tuseme Demokrasia ni Kazi. Demokrasia sio lelemama.
Ndg. Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
18 Disemba 2011

No comments:

Post a Comment