Hakika
kila chenye mwanzo hakikosi mwisho, na kila mwisho wa jambo moja huwa mwanzo wa
jingine. Ingawa huenda ni mapema sana kwangu kutoa tafakuri kamili ya muhula
wangu katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, hapana shaka
kabisa kuwa nafasi hiyo imenipa uzoefu maridhawa. Namshukuru Katibu Mkuu BAN
Ki-moon kwa kunipa fursa hii, kuniamini na kwa ushirikiano mkubwa wakati
wote wa utumishi wangu.
Kukitumikia
chombo hiki cha kimataifa kwa muda wa miaka mitano na nusu mfululizo ni heshima
ya pekee ambayo daima nitaienzi kama kilele kimojawapo cha maisha
yangu ya utumishi wa umma. Kila siku niliyoitumia katika Umoja huo
ilikuwa ni darasa la kusukuma mbele mipaka ya ujuzi na elimu. Nimepata
kufahamu mengi zaidi kuhusu Shirika lenyewe; kuhusu dunia na watu wake, lakini
pia kufahamu ukomo wa uwezo wa Umoja wa Mataifa katika kushughulikia changamoto
mbali mbali zinazoikabili dunia yetu.
Utumishi
wangu katika Umoja wa mataifa ulikuwa fursa adhimu iliyonipa uzoefu wa pekee.
Kazi hii imeujaza moyo wangu na unyenyekevu wa dhati kwani niliingia Umoja wa
Mataifa wakati ambapo dunia inachagizwa na madhila
makubwa makubwa yakiwemo maradhi, umaskini wa kupindukia, kutokuwapo kwa
usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji
kwa wanawake na watoto; na changamoto nyingine nyingi. Kwa muktadha huu
ilikuwa fursa ya pekee kuchangia juhudi za pamoja za kuimarisha Umoja wa
Mataifa katika kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mazingira
magumu ya kimataifa yaliyojaa changamoto za kipekee kabisa.
Daima
nitaendelea kushukuru na kuthamini kwa dhati jinsi Mhe. Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, Serikali na Watanzania wenzangu walivyonitia moyo na kunienzi katika
kipindi chote nilichokuwa Umoja wa Mataifa. Familia yangu, ndugu na marafiki
walikuwa karibu nami kwa dua na kunitia nguvu wakati wote wa utumishi
wangu. Nawashukuru sana.
Hapana
shaka kazi yangu katika Umoja wa Mataifa imeniwezesha kufahamiana
kwa karibu na viongozi wengi wa kimataifa na pia watu mbali mbali
waliopata mafanikio makubwa duniani. Nimeweza kufahamu kwa undani thamani
ya michango yao katika kujenga amani na ustawi wa dunia.
Zaidi
ya yote, sitasahau hisia nilizopata kila nilipokutana na watu wanyonge
waliokuwa wanahitaji msaada wa Umoja wa Mataifa. Nitakumbuka daima
tabasamu ya mwanamke mmoja niliyekutana naye katika moja ya ziara zangu barani
Afrika nilipotembelea zahanati mojawapo kati ya kadhaa zinazofadhiliwa na Umoja
wa Mataifa. Mama huyo mwenye watoto sita, alikuwa amekikumbatia kitoto chake
kimoja kilichokuwa nyonde nyonde; lakini alikuwa na tabasamu iliyojaa faraja na
matumaini kwa kuwa alikuwa amefanikiwa kupata bure dawa za kunusuru maisha ya
mwanawe.
Maendeleo
Nafasi
ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa iliasisiwa na Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa mwaka 1997 kwa madhumuni ya kuongeza ufanisi wa utendaji
wa Sekretariati na kuimarisha uongozi wa Umoja Mataifa katika medani za
uchumi na maendeleo ya jamii. Majukumu ya Naibu Katibu Mkuu yaliongezeka
kadri Shirika lilivyokuwa linapanua shughuli zake. Hatimaye Naibu Katibu Mkuu
akakabidhiwa jukumu la kuoanisha na kuratibu idara zote zilizo chini ya mwavuli
wa Umoja wa Mataifa. Jukumu hili lilikuwa na manufaa makubwa, hususan
tulipoingia katika utekelezaji wa dhana ya “Huduma ya Pamoja ” (Delivering as
One – DaO) ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi zetu hususan za
maendeleo.
Kwa
bahati nzuri, ninamaliza kipindi changu kukiwa na maendeleo mazuri yanayotokana
na jitihada za kimataifa za kupambana na umaskini. Takwimu za kuaminika za hivi
karibuni zinatuambia kuwa juhudi zetu za kupunguza idadi ya watu maskini
duniani kufikia angalau nusu ya viwango vya sasa zimeanza kuzaa matunda.
Taarifa hii ni ya kutia moyo licha ya ukweli kwamba dunia inapitia dhahama
kubwa ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote katika miaka ya hivi karibuni.
Pamoja na majukumu mengine,nguvu zetu tulizielekeza zaidi kwenye kufanikisha
malengo ya maendeleo ya milenia na malengo mengine ya maendeleo yaliyokubaliwa
kimataifa. Nilihamasika sana na dhamira waliyoionesha wadau na washirika wetu
wa maendeleo: serikali, mashirika ya kiraia na mashirika ya biashara. Kwani
wote kwa pamoja waliyatumia malengo hayo kama kilingo cha msingi katika
kutokomeza umaskini.
Katika
kufanikisha utekelezaji madhubuti wa malengo ya maendeleo ya milenia nilipewa
jukumu la kukamilisha ahadi ya Katibu Mkuu aliyoitoa kwa nchi wanachama ya
kuunda Mfumo Kamilifu wa Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs
Integrated Implementation Framework ).
Ninaona
fahari kwamba naondoka Umoja wa Mataifa mfumo huu ukiwa umekamilika ambapo
Katibu Mkuu aliuzindua mwezi Juni mwaka huu. Kwa mara ya kwanza mfumo huu
umeweka utaratibu ambao utauwezesha Umoja wa Mataifa na wadau wote kufuatilia
mwenendo wa utekelezaji wa ahadi za kisera na kifedha. Hapana shaka
utaratibu huu utaongeza uwajibikaji wa wadau na upimaji sahihi wa hatua za
maendeleo.
Malengo
ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) Barani Afrika
Kwa
mwelekeo huo huo, Katibu Mkuu alizindua Jopo la Viongozi la Kuhimiza
Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia Barani Afrika (MDG Africa
Steering Group) mwezi September 2007. Kikundi hiki kinajumuisha taasisi
zote kuu duniani zilizo mstari wa mbele katika kuchochea kasi ya maendeleo ya
Afrika. Nilipata bahati ya kukiongoza kikosi-kazi (MDG Africa Working
Group) kilichokuwa mhimili wa Jopo hilo la viongozi. Baada ya miaka
mitano ya majadiliano ya kina, Jopo hilo likiongozwa na Katibu Mkuu limetoa
mapendekezo kamambe ya utekelezaji. Endapo mapendekezo haya
yatazingatiwa basi yatakuwa nyenzo muhimu ya kuweka sera na mikakati
madhubuti itakayosaidia maendeleo katika nchi husika na duniani kwa
ujumla.
Napenda
kutoa mwito kwa wadau wote kuyapa umuhimu mapendekezo haya.
Ninafahamu
kwamba tathmini kamili ya mafanikio ya utekelezaji wa Malengo ya
Maendeleo ya Milenia imepangwa kufanyika Septemba mwaka 2013. Hata
hivyo tayari tunaweza kusema kuwa Malengo haya yameleta mabadiliko chanya
katika maisha ya watu wa kawaida sehemu nyingi duniani, hususan barani
Afrika. Ni dhahiri kuwa jamii nyingi zimenufaika na utekelezaji wa
malengo ya maendeleo ya milenia sio kwa kufanyiwa hisani bali kwa wao wenyewe
kuwa na mikakati maalum ya kupiga hatua madhubuti za kujiletea maendeleo
stahimilivu na yaliyolenga kuleta usawa baina ya watu.
Mkutano
wa Rio + 20
Ni
jambo la kutia moyo kwamba maendeleo shirikishi na yenye kuleta usawa ni baadhi
ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano wa Rio +20 uliomalizika hivi
karibuni. Suala hili litachukua nafasi kubwa pia katika kuandaa mfumo wa
maendeleo unaotarajiwa baada ya mwaka 2015, mwaka uliokusudiwa
kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilipokabidhiwa jukumu la
kuratibu maandilizi ya ushiriki wetu kwenye mkutano wa Rio+20 nilitiwa moyo na
nia ya dhati ya mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kubuni mkakati wa pamoja wa
kutekeleza maazimio ya Rio+20. Napenda kuzishukuru nchi wanachama kwa kufikia
makubaliano katika masuala mengi yaliyojadiliwa Rio licha ya changamoto nyingi
zinazotokana na mtikisiko wa uchumi duniani. Ninafurahi kwamba maazimio ya
mkutano huu yatachangia upatikanaji wa maendeleo stahimilivu, shirikishi na
yenye kuleta usawa na hususan kuhakikisha kunakuwa na mustakabali mzuri kwa
wanawake na wasichana.
Uwezeshaji
wa wanawake na usawa wa kijinsia
Tukirejea
kwenye suala hili, hata baada ya Mkutano wa Rio + 20 tutawajibika kuendelea na
juhudi za uwezeshaji wa wanawake na kuleta usawa wa kijinsia. Wakati wa
utumishi wangu Umoja wa Mataifa tumefanya bidii kubwa na kutumia muda mwingi
kushughulikia suala hii. Tumetumia hadhi na ushawishi wa ofisi yetu kupaza
sauti za wanawake na wasichana na kukuza ushiriki wao katika jamii. Tumeendesha
kampeni za kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana.
Tumezihimiza
mamlaka katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutunga sera na sheria
zinazozingatia haki za wanawake na usawa wa kijinsia, na tumetaka wapewe fursa
kushika nafasi za uongozi katika jamii. Ndiyo maana kwa upande wetu
hatukuweka koleo chini hadi pale tulipokamilisha uanzishwaji wa idara inayojulikana
kwa kifupi kama “UN Women” mnamo Julai 2010. Hii ni idara ya Umoja wa
Mataifa iliyoundwa kwa madhumuni ya kuongoza masuala ya wanawake na usawa
wa kijinsia kwa umakini na ufanisi zaidi kuliko hapo awali. Tumefanya jitihada
hizi kwa kuamini kuwa hakuna uamuzi wowote ule, uwe mdogo au mkubwa, unaofanywa
na Umoja wa Mataifa bila ya kuzingatia maendeleo na ustawi wa wanawake na
wasichana.
Huduma
ya Pamoja
Kwa
upande mwingine ninapenda kuwapongeza kwa dhati wenzangu wote waliomo katika
utumishi wa Umoja wa Mataifa,wake kwa waume,walioutumia ujuzi na weledi wao
wote kuchangia maendeleo ya nchi na jamii tunazozihudumia. Natoa shukrani za
pekee kwa wale wote waliopo kwenye ofisi na vituo vya Umoja wa Mataifa nje ya
Makao Makuu na ambao wanafanya kazi katika mazingira magumu na yenye changamo
nyingi. Hao wote wanadhihirisha umuhimu wa kuwapo kwa Shirika hili kama chombo
cha kuhimiza maendeleo katika ngazi zote za kitaifa, kikanda na
kimataifa. Katika kutekeleza dhana ya “Huduma ya Pamoja” (Delivering as One)
Waratibu Wakaazi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na mchango muhimu
sana.Uratibu wao umeongeza ubora na wepesi wa utoaji huduma kwa nchi
wanamowakilisha Shirika. Hatuna budi kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa katika
kufanikisha dhana ya “Huduma ya Pamoja”. Ni dhahiri kwamba uwezo wa
nchi mwanachama kumiliki mchakato wa maendeleo yake unakuwa imara
zaidi pale ambapo kuna mtiririko mzuri wa huduma za Umoja wa Mataifa na
fursa za kukuza ushirikiano endelevu na wadau wengine wa maendeleo. Wakati
uamuzi rasmi kuhusu maendeleo ya dhana hii ukisubiri kukamilika kwa majadiliano
ya nchi wanachama, ninaamini kwa dhati kuwa utaratibu wa kutoa “Huduma ya
Pamoja” kupitia mpango mmoja uliokubaliwa na wote ni mwelekeo sahihi na wenye
tija.
Nchini
mwetu Tanzania, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakifanya kazi kwa
ushirikiano wa karibu sana toka mwaka 2011 kupitia mpango mmoja uitwao “Mpango
wa Umoja wa Mataifa wa Kusaidia Maendeleo” (United Nations Development Plan
– UNDAP). Mpango huu unakwenda sambamba na mwaka wa fedha wa Serikali yaani
Julai 1 hadi Juni 30 na kwa mantiki hiyo kuuwezesha kuzingatia vipaumbele vya
Serikali. Kupitia mpango huu Umoja wa Mataifa umejiwekea utaratibu wa kujipima
na kujitathmini ambao unatoa fursa kwa hatua za haraka kuchukuliwa inapobidi. Utaratibu
huu unapatikana kwenye tovuti. Kwa upande wa uendeshaji, mfumo huu wa utendaji
kazi kwa pamoja umetuwezesha kutekeleza majukumu mengi kwa kutumia raslimali
chache ambapo“ziada” iliyopatikana imeelekezwa kwenye shughuli nyingine za
maendeleo.
Afya
ya Jamii
Katika
eneo la afya, ambamo wanawake na watoto ndiyo wanaathirika zaidi, hatua muhimu
zinachukuliwa kupunguza vifo na kuhakikisha kwamba kila mwanamke na kila mtoto
anakingwa na maradhi, hususan kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto. Tukiwa Nairobi Aprili mwaka 2011, Katibu Mkuu Ban
Ki-moon, Michel Sidibe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) pamoja nami tulishuhudia mfano hai wa
jitihada za Umoja wa Mataifa. Tulipata fursa ya kukutana na mwanamke
aliyeathirika na virusi ambaye alijaaliwa kupata mapacha watatu waliozaliwa
bila ya maambukizi. Nikiwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa
iliyoshughulikia taarifa na uwajibikaji katika masuala ya afya ya mama na mtoto
(Commission on Information and Accountability on Women’s and Children’s
Health) ambayo iliendeshwa kwa umahiri na Rais Kikwete wa Tanzania na
Waziri Mkuu Harper wa Canada, nina imani kwamba jumuiya ya kimataifa hivi
sasa imepata mfumo madhubuti utakaohakikisha kwamba kunakuwa na ufuatiliaji,
usimamizi na uwajibikaji kuhusu afya ya mama na mtoto. Hakuna shaka kwamba
mfumo huu utafikia hatua ya utekelezwaji siku za hivi karibuni.
Hali
kadhalika, kazi nzuri imekuwa ikifanywa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa
Shirika la Mpango wa Uzazi Duniani (UNFPA), Babatunde Osotimehin, na Margaret
Chan, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kuboresha afya ya
mama na mtoto. Matokeo ya jitihada za wenzangu hawa yalikuwa chachu ya
utekelezaji wa majukumu ya Naibu Katibu Mkuu katika nyanja zote za maendeleo.
Ama kwa hakika matunda ya kazi zao yanaimarisha imani yangu kuwa Umoja wa
Mataifa ni Shirika lenye umuhimu mkubwa; na kwamba mchango wetu, japo mdogo,
unasaidia sana katika kufikia malengo ya maendeleo ya milenia. Nilijawa na
imani kama hiyo nikiwa katika ziara nyingine za kikazi. Kwa mfano nikiwa
Montevideo, Uruguay, Novemba 2011, pamoja na wenzangu Michelle Bachelet,
Helen Clark na Alicia Barcena, tulisimama kidete kuunga mkono kampeni
ya kitaifa ya kupiga vita vitendo vya ukatili kwa wanawake.
Nilipozuru
Haiti mwezi Aprili2010, miezi michache baada ya tetemeko ambalo lilikuwa kubwa
kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini humo kwa kipindi cha takriban karne moja,
nilikutana na watu ambao walikuwa wameathirika vibaya sana: waliopoteza familia
nzima, waliopata ulemavu wa maisha, waliopoteza mali zao zote! Lakini bado watu
hawa walikuwa na nyuso za matumaini wakitarajia mchango wa Umoja wa Mataifa na
wa wadau wengine wa jumuiya ya kimataifa. Mnamo Novemba 2010 tulizuru Laos,
ambako Umoja wa Mataifa unashirikiana kwa karibu na Serikali na wadau wengine
wengi katika utoaji wa misaada muhimu ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuisaidia
Laos kupambana na janga la mabaki ya mabomu ya “cluster munitions”.
Hii
ni mifano michache tu inayojibu hoja za wakosoaji wa Umoja wa Mataifa.Ujumbe
wangu kwao ni huu: wanyonge na wenye kutaabika sehemu zote duniani ni mashuhuda
na watetezi wakubwa wa Umoja wa Mataifa. Kwa wanyonge na wahitaji walio
wengi Shirika hili ni nguzo ya kutumainiwa katika jitihada zao za kila siku za
kujiletea maisha yenye utu na heshima.
Mageuzi
katika menejimenti na usimamizi wa mabadiliko
Ukweli
huu haumaanishi kuwa Umoja wa Mataifa hauna kasoro au upungufu. La hasha! Ndiyo
maana wakati wa utumishi wangu tulijielekeza kikamilifu kwenye kuboresha
masuala ya utawala, uendeshaji na namna tunavyofanya kazi.
Ni
wazi kwamba hivi sasa Umoja wa Mataifa umebadilika kutoka chombo cha huduma za
mikutano na kuwa mtendaji mwenye majukumu muhimu nje ya kumbi za mikutano. Kwa
ushirikiano na msaada maridhawa wa wafanyakazi wenzangu, tulijikita katika
kuhamasisha mabadiliko ya kiutendaji katika Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja
na kujenga desturi ya uwajibikaji, uadilifu na kufanya kazi kwa tija zaidi huku
tukitumia rasilmali chache.
Ilitubidi
pia kuweka mifumo thabiti ya kusimamia mabadiliko yaliyokuwa yakijitokeza.
Katika kufanya hivyo tulitambua wazi kwamba hakukuwa na njia ya mkato wala njia
mbadala ya kuliimarisha Shirika letu na kulifanya liwe la kisasa zaidi katika
kutekeleza majukumu yake.Tulihakikisha kwamba utendaji kazi wetu unakwenda
sambamba na changamoto zilizopo, lakini pia tulizingatia ufinyu wa bajeti,
misimamo tofauti na wakati mwingine inayaokinzana ya nchi wanachama wa
Umoja wa Mataifa. Katika hali hii ilitulazimu kuwa wabunifu zaidi
ili kuleta muafaka baina ya nchi wanachama na kuhakikisha kwamba
raslimali chache zilizopo zinatoa tija kubwa zaidi.
Wafanyakazi
ndiyo rasilmali kubwa kupita zote. Hivyo kila tulipoendelea na jitihada za
kuboresha Shirika ilitubidi kuwekeza vilivyo kwa wafanyakazi wa Umoja wa
Mataifa kwa kuwapatia fursa za mafunzo na msingi imara wa maendeleo yao kazini.
Ni jambo lililo dhahiri kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanatekeleza
majukumu yao katika mazingira hatarishi na yenye kubadilika mara kwa mara.
Tunafahamu, tena kwa uchungu mkubwa, kuwa Bendera ya Umoja wa Mataifa
- “bendera ya bluu” – hivi sasa si kinga tena.
Haituhakikishii usalama kwani wengi wa watumishi wetu mahiri wamekuwa wahanga
wa matukio ya kikatili ya ugaidi. Nilishuhudia tukio la aina hii huko Abuja,
Nigeria, ambako watumishi wenzetu walipoteza maisha kutokana na shambulio la
kigaidi la tarehe 26 Agosti 2011. Na mara nyingi wenzetu wanapotangulia mbele
ya haki, wapendwa wao wanaachwa katika hali ngumu ya maisha. Ni faraja kubwa
kwangu kuwa miongoni mwa masuala ambayo tuliyasimamia kabla ya kumaliza
utumishi wangu ni kuanzisha mchakato wa kubaini namna bora ya kuwasaidia
wahanga wa majanga hayo pamoja na familia zao.
Utawala
wa sheria
Mojawapo
ya majukumu ya Umoja wa Mataifa ni kukuza sera zinazolenga kulinda haki za
binadamu na kuendeleza utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
Leo hii, nchi nyingi zimelipa kipaumbele suala la kuimarisha utawala wa
sheria, hususan kufuatia umuhimu wake katika ajenda za ujenzi wa amani
(peace-building) na maendeleo stahimilivu. Kwa mantiki hiyo, nilifurahi
nilipopata fursa ya kusimamia ujenzi wa mfumo madhubuti wa sera na mwongozo wa
utekelezaji wa shughuli za utawala wa sheria nikishirikiana na nchi wanachama.
Kwa upande wao nchi wanachama zimepanga kufanya mkutano wa ngazi ya juu wakati
wa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba 2012. Nia kubwa ni
kuendeleza jitihada katika suala hili ili kukuza heshima ya watu wote duniani
na kujenga amani kati ya mataifa.
Hitimisho
Japokuwa
muda wangu wa utumishi katika Umoja wa Mataifa umefikia tamati, naamini hakuna
tamati katika utekelezaji wa malengo, misingi na maadili ya Umoja wa
Mataifa. Ili mradi bado kuna umaskini duniani na mahitaji ya chakula;
bado kuna changamoto ya kutunza utu na heshima ya binadamu na haja ya
kuimarisha amani duniani basi hakika nitaendelea kuunga mkono jitihada, misingi
na malengo ya Umoja wa Mataifa popote pale nitakapokuwa. Kwani ni dhahiri
kwamba njia bora ya kukabiliana na changamoto kubwa zilizo mbele yetu ni
kujenga ubia na ushirikiano wa karibu baina ya serikali, asasi za kiraia,
wafanyabiashara, mashirika ya hisani, taasisi za kitaaluma na watu binafsi.
Aidha,
ninaaamini kuwa vijana, kizazi ambacho kina kila sababu ya kuwa na kiu ya
kuishi kwenye dunia yenye utu, usawa, haki na amani, watauchukulia Umoja wa
Mataifa kuwa mbia wa kuaminika katika kujenga mustakabali wao.
Asha-Rose Migiro
No comments:
Post a Comment