MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi
jijini Dar es Salaam, imesema mgomo wa walimu ni batili kwasababu haukuzingatia
matakwa ya kifungu cha 84(1),(2) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazi ya mwaka
2004 na uliandaliwa kwa dhamira mbaya.
Jaji Sophia Wambura wa mahakama hiyo alitoa uamuzi huo leo saa 9:14-37 alasiri
huku ukumbi wa wazi wa mahakama hiyo ukiwa umefurika walimu ambapo katika
uamuzi wake huo pia aliwataka walimu wote kurejea mara moja kazini. Jaji
Wambura alisema asikiliza kwa makini hoja za mawakili waandamizi wa serikali
Pius Mboya na Obadia Kameya ambao walikuwa wakiwawakilisha walalamikaji katika
maombi hayo madogo namba 96/2012 yaliyoletwa chini ya hati ya dharura na Katibu
Mkuu Kiongozi,Katibu Mkuu Ofisi ya rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ya mdaiwa ambaye ni Chama cha Walimu
Tanzania(CWT) ambao walikuwa wakiwakilishwa na wakili wa kujitegemea Gabriel
Mnyele. Jaji Wambura alisema mgogoro uliowasilishwa mbele yake na walalamikaji
ni kwamba wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa mgomo wa walimu ni batili wakati
wakili wa CWT ,Mnyere alidai mgomo huo ni halali kwa sababu umekidhi matakwa ya
sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini. Jaji huyo alisema mahakama yake imefikia
uamuzi wa kutofautiana na zoezi la upigaji kura za kuunga mkono mgomo ambalo
liliendeshwa na CWT ambapo asilimia 97 ya walimu waliinga mkono kuanza kwa
mgomo kwasababu zifuatazo: “Mosi, zoezi lile la upigaji kura lilikuwa
likiwadanganya wanachama wa CWT kuwa zoezi hilo limeendeshwa rasmi na kwa
mujibu wa sheria,zoezi lile halikukidhi matakwa ya sheria kwasababu wanachama
wake walikuwa hawajaelewa na viongozi wa chama hicho madhara ya kufanya mgomo
huo,zoezi lile halikufuata taratibu; “Noti ya kugoma iliyotolewa na CWT Julai
27 mwaka huu saa tisa alasiri wakati zoezi la upigaji kura zile lilikuwa bado
halijafanyika na kwasababu hiyo zoezi lile likikuwa batili: “Kwa mdaiwa(CWT)
kushindwa kufuata matakwa ya kifungu cha 42 na 43 cha Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini,ni wazi taratibu zote walizozifanya za kupiga kura ya kuunga
mkono mgomo na kugoma mdaiwa alizifanya akiwa na dhamila mbaya kwani wajumbe wa
chama hicho hakuwa na makubaliano ya jinsi mgomo utakavyoendeshwa na
kusimamiwa”alisema Jaji Wambura huku baadhi ya walimu wakiwa wamejiinamia.
Alisisitiza kuwa CWT imeitisha mgomo huo ikiwa na dhamira mbaya kwasababu ni
CWT ndiyo alikataa kuendelea na mazungumzo na mwajiri wake badala yake
akaanzisha mgomo wakati Julai 27 mwaka huu, pande zote katika hizo zilifika
mbele yake kuomba na upande wa mlalamikaji ukaomba mahakama itoe amri ya kutaka
pande zote zisiendelee na jambo lolote hadi mahakama itakapowasilikiliza lakini
cha kushangaza siku hiyo hiyo saa tisa alasiri CWT ilienda kutoa noti ya kuanza
mgomo kwa walimu nchi nzima ndani ya saa 48 wakati kulikuwa na amri ya mahakama
iliyozitaka pande zote kutoendelea kufanya jambo lolote linalohusiana na kesi
hiyo ambapo mgomo huo batili ulianza rasmi nchi nzima kuanzia Jumatatu ya wiki
hii na hadi sasa unaendelea. “Kwa maelezo hayo hapo juu nasisitiza mgomo huo ni
batili kwani haujakidhi matakwa ya kifungu cha 84(1),(2) cha Sheria ya Ajira na
Mahusiano Kazini ya mwaka,na mgomo uliondeshwa kwa siku tatu sasa ni batili na
ninaamuru mgomo huo usitishwe mara moja na walimu wote warejee kazini na kwa
kuwa mdaiwa aliitisha mgomo huo kwa mkutumia taarifa kwa vyombo vya habari pia
naamuru kiongozi aliyetoa taarifa hiyo ya mgomo aende tena kwenye vyombo vya
habari akatangaze kuwa mgomo waliokuwa wakiufanya ni batili na kuwataka walimu
warejee kazini mara moja na mahakama hii imemshangaa sana wakili Mnyere kwa
kushindwa kuwashauri wateja wake mapema kwamba mgomo waliokuwa wakiundesha
ulikuwa umekiuka sheria” alisema Jaji Wambura. Aidha pia naiamuru CWT kulipa
gharama na fidia kwa kipindi chote ambacho wanafunzi wamekosa vipindi kwaajili
ya mgomo huo batili na kama pande zote zinaona kuna hata ya kurudi meza ya
majadiliano zilirudi kwenye meza ya majadiliano na zimualike mtaalamu wa sheria
za kazi awasaidie kufikia mwafaka. Baada ya hukumu kutolewa,baadhi ya viongozi
wa CWT waliwaomba waandishi wa habari waje nje ya mahakama kwani kutakuwa na
mkutano lakini hata hivyo waandishi walipofika nje ya viwanja hivyo mahakama
walimkuta Rais wa chama cha walimu,Gration Mkoba akiwa amenyongonyea na hata
alipotakiwa atoe tamko ni lini atatekeleza amri ya mahakama iliyomtaka aende
kwenye vyombo vya habari autangazie umma kuwa mgomo alioutisha ni batili na
awatake walimu warudi kazini aliishia kusema leo atafanya mkutano na waandishi
wa habari na kwa upande wa wakili wao Mnyere alisema amekubaliana na uamuzi huo
wa mahakama.
No comments:
Post a Comment