Rais akiongea na wahariri jana Ikulu |
HOTUBA YA MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 JULAI, 2012
Ndugu Wananchi;
Naomba
nianze kwa kuomba radhi kwa kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi wa saba, leo tarehe
01 Agosti, 2012 badala ya jana tarehe 31 Julai, 2012. Hii ni kwa sababu ya
msiba uliotukuta katika familia na mimi kwenda Lindi kushiriki maziko ya
marehemu wetu. Tofauti na miezi iliyopita leo, pamoja na hotuba ya kawaida ya
mwisho wa mwezi nimetoa fursa kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini
kuniuliza maswali nami kujibu. Kwa upande wangu nina mambo matatu ambayo
nitayazungumzia leo.
Ajali ya Kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la kwanza ni ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012. Meli
hiyo ilikuwa na watu290, wakiwemo mabaharia 9, abiria watu wazima 250 na watoto
31. Juhudi za uokoaji zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli hiyo
kupatikana. Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM walishiriki pamoja na
meli na watu binafsi katika uokoaji. Waokoaji walifanikiwa kuwapata ndugu zetu
146 wakiwa hai na maiti 126 hadi tarehe 27 Julai, 2012. Kwa maana hiyo basi,
watu 18 hawajulikani walipo na inahofiwa kuwa nao pia hawako hai. Huenda
wamezama pamoja na meli au walizama baharini lakini miili yao haikuweza
kupatikana.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kurudia kutoa mkono wa rambirambi na pole nyingi kwa wale
wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ile. Nampongeza sana
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein na viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa
kazi kubwa na nzuri waliofanya kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma
walizotoa kwa waliokolewa, waliojeruhiwa na waliofariki. Kwa wale ambao
walikuwa wenyeji wa Unguja na Pemba, SMZ ilitoa sanda na usafirishaji wa maiti
mpaka makwao kwa mazishi. Kwa wale wasiokuwa na ndugu Serikali ilibeba jukumu
la kuwazika kule Kama, Kusini Unguja.
Natoa
pongezi za pekee kwa wale wote walioshiriki katika uokoaji kwani juhudi zao
ziliwezesha ndugu zetu wengi kusalimika na maiti nyingi kupatikana.
Ndugu
Wananchi;
Kutokea
kwa ajali ile kumetonesha jeraha la huzuni, majonzi na mashaka makubwa
yaliyolipata taifa letu miezi 11 iliyopita kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya
MV Spice Islander. Katika mkutano maalum wa Baraza la Usalama wa Taifa
niliouitisha tarehe 20 Julai, 2012 kuzungumzia ajali ya MV SKAGIT tulifanya
mapitio ya utekelezaji wa maagizo yetu ya mkutano wa tarehe 11 Septemba, 2011
kufuatia ajali ya MV Spice Islander. Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji
umekuwa mzuri kwa upande wa mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani
SUMATRA, Zanzibar Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili.
Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni mzuri kwa mambo yote muhimu ambayo
Baraza liliagiza wafanye hivyo. Pamoja na hayo Baraza limetaka ushirikiano huo
uzidishwe na kuimarishwa.
Kwa
mfano, Baraza limefurahishwa na kupongeza kitendo cha mamlaka hizo kutumia Dar
es Salaam Maritime Institute kwa ushauri kuhusu ubora wa meli na huduma za
usafirishaji majini. Baraza limeagiza vyombo hivyo viwe na hadidu za rejea
zinazofanana kwa vigezo vya ubora ili nchi yetu iwe na viwango vinavyofanana
vya ubora wa meli na huduma za usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za Muungano.
Bahari ni moja na vyombo vinahudumia watu wale wale, kuwa na vigezo tofauti vya
ubora wa meli na viwango vya huduma ni jambo lisilostahili kuwepo tena, ni la
hatari. Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri wa meli zilizokwishatumika
zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Aidha,
Baraza limerudia kuagiza pawepo na usimamizi makini zaidi kuhusu upakiaji wa
mizigo na abiria. Mamlaka husika, yaani SUMATRA, ZMA na maofisa wa bandari
wahakikishe kuwa uwezo wa meli uliohakikiwa na kutambuliwa unaheshimiwa
ipasavyo. Pia, meli zikaguliwe mara kwa mara na vigezo vifanane.
Ndugu
Wananchi;
Pamoja
na hayo, Baraza la Usalama wa Taifa limeona kuwa wakati umefika kwa Serikali
yetu kuwa na Coast Guards, yaani kikosi maalum cha uokoaji na usalama majini.
Aidha, Baraza limetaka hatua za makusudi zichukuliwe kuimarisha KMKM na Police
Marines. Mwisho, Baraza lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza
ajali ile kama ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice Islander.
Utafutaji na Uchimbaji Gesi Nchini
Ndugu
Wananchi,
Jambo
la pili ninalopenda kulizungumzia leo ni kuhusu maendeleo ya sekta ya gesi
asili nchini. Juhudi za kutafuta mafuta nchini zilianza mwaka 1952 na mwaka
1954 wakati kampuni ya BP ilichimba kisima cha kwanza kule Mafia. Bahati mbaya
kisima hicho hakikuzaa matunda yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta
zikafifia kabisa mwanzoni mwa miaka ya 1960. Miaka kumi baadae, juhudi hizo
zilianza upya na kuendelea kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali hadi sasa.
Katika miaka ya hivi karibuni juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni
kadhaa ya kimataifa yakiwemo makubwa na madogo.
Ndugu
Wananchi;
Tangu
mwaka 1954, mpaka sasa visima 61vimechimbwa, kati ya hivyo, gesi asili
imegunduliwa katika visima 22, visima 14 vya nchi kavu na maeneo ya maji mafupi
na visima 8 vya bahari ya kina kirefu. Hatujabahatika kupata mafuta lakini
tumefanikiwa kupata gesi asili katika maeneo kadhaa baharini na nchi kavu
katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizopo kutokana na visima vilivyochimbwa mpaka sasa, akiba
ya gesi asili iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo trilioni
25.4 – 28.9. Yapo matumaini makubwa ya gesi nyingi zaidi kugundulika katika
miaka michache ijayo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta
na hasa gesi baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo
18. Baada ya ugunduzi wa kwanza wa gesi mwaka 2010, shughuli za utafutaji sasa
zimepamba moto na zimekuwa na mafanikio. Naamini gesi nyingi zaidi itaendelea
kupatikana.
Fursa za Maendeleo
Ndugu
Wananchi;
Kwa
kiasi cha gesi asili kilichokwishagunduliwa na kwa matumaini yaliyopo ya gesi
zaidi kupatikana kunaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi za kutumainiwa duniani
kwa upatikanaji wa gesi asili miaka michache ijayo. Hali hiyo inaipa nchi yetu
fursa kubwa ya kuweza kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda
si mrefu kutoka sasa.
Gesi
asili ni rasilimali inayoweza kutumika kuzalisha mbolea na hivyo kusaidia
katika kuendeleza kilimo nchini kwa kurahisisha upatikanaji wake na kuwa ya bei
nafuu. Gesi asili inaweza kutumika kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi
kupata umeme wa kutosha na kuwepo ziada ya kuuza nje. Hivi sasa, katika gridi
ya taifa megawati 350 za umeme zinatokana na gesi asili na hata lengo letu la
kuzalisha megawati 3,500 ifikapo maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili
kuwezesha hilo kutimia. Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es
Salaam una shabaha hiyo.
Ndugu
Wananchi;
Vile
vile, gesi asili inaweza kutumika kutoa nishati viwandani badala ya kutumia
mafuta na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji. Watu majumbani wanaweza
kutumia gesi asili kupikia hivyo kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na
kuni. Inapunguza gharama za maisha na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa
kupunguza ukataji wa miti. Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana TPDC
inatekeleza mradi wa kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi majumbani
katika jiji la Dar es Salaam.
Jambo
lingine muhimu kuhusu rasilimali hii ni kwamba tukiuza nje gesi nchi yetu itapata
mapato mengi tena ya fedha za kigeni. Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya
Serikali yataongezeka sana, hivyo kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake
vizuri zaidi. Kama matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa kichocheo
kikubwa cha kukuza uchumi wa nchi. Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo
kusaidia kuwaondoa wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini tulionao
sasa.
Changamoto Muhimu
Ndugu
Wananchi;
Pamoja
na ukweli kwamba kuwa na gesi asili nyingi kunaipa nchi yetu fursa kubwa ya
kujiletea maendeleo, zipo pia changamoto zake. Hatuna budi kuzitambua na
kuzitafutia ufumbuzi ili gesi iweze kunufaisha ipasavyo nchi yetu na watu wake.
Changamoto zipo nyingi lakini kubwa zipo za namna tatu.
Changamoto
ya kwanza ni ile ya kujenga uwezo wetu wenyewe wa kudhibiti shughuli
zinazofanywa na makampuni ya mafuta ili tuhakikishe kuwa tunapata malipo
yanayostahili. Inatulazimu tuwe na wataalamu wetu wazalendo wa fani za taaluma
zihusuzo gesi kama vile uhandisi, kemia, jiofizikia, uhasibu, ukaguzi na
sheria. Tusipojenga uwezo wetu wenyewe kwenye maeneo hayo kuna hatari ya
kudhulumiwa na kupata hasara. Pengine ipo haja ya kuwa na chombo maalum kwa
ajili hiyo kama tulivyofanya kwa mafanikio kwa upande wa dhahabu.
Changamoto
ya pili ni ile ya kupata Watanzania wengi wenye ujuzi na taaluma zinazohitajika
na soko la ajira la sekta ya gesi. Tusipofanya hivyo makampuni yataajiri watu
hao kutoka nje na hivyo kufanya Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira
zilizopo.
Ndugu
Wananchi,
Kwa
changamoto hizi mbili, jawabu lipo kwenye elimu na mafunzo tunayotoa kwa vijana
wetu katika shule, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu. Kwanza kabisa
lazima tuboreshe elimu ya sayansi na hisabati katika shule zetu za msingi na
sekondari. Katika vyuo vya ufundi tutoe mafundi mchundo wa taaluma
zinazohitajika na tasnia ya gesi na mafuta. Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo
vikuu nako wafundishe wataalamu wa fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa
gesi na mafuta, uendelezaji wa mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na
gesi, uhasibu na ukaguzi wa mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi
na mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.
Ndugu
Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa tayari tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinajiandaa kuanza kutoa mafunzo yaChemical and
Environmental Lab for Oil and Gas na fani yaExploration and Production Software
Technology katika mwaka huu wa masomo. Chuo cha Madini Dodoma kitaanza kutoa
mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia Septemba mwaka huu. Chuo
Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha, na
Chuo cha Teknolojia cha Mbeya na kile cha Dar es Salaam pia wameanza kufundisha
mitaala hiyo. Aidha, VETA Makao Makuu na VETA Mtwara nao wanafundisha masomo
yahusuyo gesi. Wizara ya Nishati na Madini itawadhamini wanafunzi 50 kutoka
Mkoa wa Mtwara kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili katika chuo cha VETA
Mtwara.
Ndugu
Wananchi;
Wizara
ya Nishati na Madini pia inatekeleza mpango mkakati wa kuwapata wataalamu wa
sekta hiyo kati ya 40-50 kati ya sasa na mwaka 2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo
ni Petroleum Geoscience, Petroleum Geophysics, Petroleum Geochemistry,
Petroleum Engineering, Petroleum Modeling, Oil and Gas economics, Oil and Gas
Accounting and Auditing na Oil and gas Legal Regimes and Contract Negotiations.
Kwa upande wake, Serikali itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za
mafunzo ili tuweze kuwapata wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba vijana
wetu wachangamkie fursa hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo wawe tayari
kuitumikia nchi yetu kwa bidii.
Kujenga Uwezo Wetu wa Kutumia Mapato ya
Gesi
Ndugu
Wananchi,
Changamoto
nyingine kubwa sana ni ile ya kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na gesi
yanatumika vizuri na kwa manufaa ya taifa na watu wake. Lazima tuanze sasa
kufikiria na kujipanga kwa ajili hiyo. Si vyema tukangojea mpaka hapo mapato
yatakapoanza kupatikana ndiyo tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamia
na kutumia mapato yatokanayo na gesi. Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na
waovu watakuwa wameanza kunufaika hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo
utakaowanyima fursa ya kuliibia taifa.
Jambo
hili ni muhimu sana kufanya kwani ipo mifano hai ya nchi zenye rasilimali
nyingi za mafuta na gesi lakini nchi na wananchi wake hawanufaiki sawia. Mauzo
yanafanyika na fedha nyingi kupatikana lakini manufaa kwa nchi na watu wake ni
madogo au hayapo kabisa. Wanaonufaika ni viongozi na baadhi ya maofisa wa umma
wanaohusika na usimamizi wa shughuli zihusuzo rasilimali hizo. Na, hata sisi
tunaweza kujikuta katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala
ya rasilimali kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.
Ndugu
Wananchi;
Zipo
nchi duniani ambazo zina usimamizi mzuri wa mapato ya rasilimali za mafuta na
gesi na kuleta baraka na neema kwa taifa na watu wake. Nchi hizo zimeweza
kuhifadhi na kutumia vizuri mapato yake kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na
kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kwa watu. Matokeo yake
ni watu wa nchi hizo kuishi maisha yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya
kupatikana kwa rasilimali hizo. Lakini, hii imewezekana kutokana na usimamizi
mzuri na matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi.
Tumeamua
kujifunza kutoka nchi za wenzetu waliofanikiwa ili na sisi tunufaike. Na sisi
tunajiandaa kutengemeza Sera ya Gesi Asili na kurekebisha Sheria ya Utafutaji
na Uzalishaji wa Mafuta na Sheria ya Menejimenti ya Mapato ya Serikali
yatokanayo na gesi zitakazotoa majibu hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo
mzuri wa usimamizi wa utafutaji na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi
na matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na gesi hiyo. Wapo wenzetu kwa mfano,
wanacho kitu kinachoitwa Sovereign Funds ambapo mapato yote huhifadhiwa na
baadae hutolewa kwa utaratibu maalum. Tunataka tujifunze kutoka kwao ili na
sisi tutengeneze chombo chetu cha namna hiyo ili tunufaike.
Ndugu
Wananchi;
Mambo
hayo tumeshaanza kuyafanyia kazi. Katika mazungumzo yangu na baadhi ya wakuu wa
nchi rafiki na mashirika ya maendeleo ya kimataifa, nimewasilisha maombi ya
kusaidiwa na kushirikiana kwa mambo mawili. Kwanza kwa kuwawezesha Watanzania
kupata mafunzo ya haraka kwa wataalamu watakaosaidia kusimamia shughuli za
utafutaji, uendelezaji na biashara ya gesi asili nchini. Pili, watusaidie kupata
watu wenye ujuzi na uzoefu ili watushauri kuhusu namna ya kutengeneza mifumo
bora ya kusimamia na kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa mifano ya wenzetu
waliofanikiwa. Nafurahi kwamba maombi yetu yamepokelewa vizuri na nchi zote na
mashirika yote ya kimataifa tuliozungumza nao. Baada ya muda si mrefu kazi
itaanza.
Mgomo wa Walimu
Ndugu
Wananchi;
Jambo
la tatu na la mwisho ni mgomo wa walimu. Pengine ni mapema kusema kwa vile
kesho Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo. Lakini napenda kuwahakikishia walimu
kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu.
Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo
mbalimbali. Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo. Athari za
kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75kwa ajili
ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25 kwa kuendeshea
Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi. Haitakuwa sawa. Ndiyo
maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao kusisitiza kugoma.
Wakati
tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu: Moja,
wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na
kazi. Pili, wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao. Nawasihi warudi
kwenye meza ya mazungumzo.
Ndugu
Wananchi;
Kabla
ya kumaliza hotuba yangu naomba nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote
nchini kheri na baraka tele kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Wakati
wote, mjiombee wenyewe kwa Mwenyezi Mungu awajaalie toba na malipo mema katika
mfungo huu. Mkumbuke pia kuiombea nchi yetu amani, upendo na mafanikio mema.
Baada
ya maneno hayo, naomba sasa niishie hapo. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.
Sasa nipo tayari kujibu maswali ya Wahariri kama yapo. Ndugu Wahariri mliopo
hapa, karibuni.
No comments:
Post a Comment