Tuesday, September 11, 2012

SIMBA FC NA AZAM FC..Nani kubeba ngao ya jamii leo?

Kikosi cha Azam FC

Kikosi cha Simba FC

SIMBA SC inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo kumenyana na Azam FC katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii, iliyopangwa kuanza saa 10:30 jioni.
Simba itakayotokea katika hoteli ya Sapphire, Kariakoo itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 3-0 na Sofapaka ya Kenya, katika mchezo wa kirafiki, Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja huo huo.

Lakini awali ya hapo, Simba ilicheza mechi tatu za kirafiki ikiwa kambini Arusha, dhidi ya Mathare United ya Kenya, JKT Oljoro ya Arusha ambazo kila moja ilishinda 2-1, kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar ya Kenya. 
Habari njema zaidi mshambuliaji hatari wa Simba SC, Emanuel Arnold Okwi alitua juzi kutoka Zambia, ambako aliichezea timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani Afrika Kusini jana na kufungwa 1-0 kwa mbinde na leo anatarajiwa kucheza. 
Okwi hajaichezea Simba mechi yoyote tangu msimu huu uanze, kutokana na pilika zake za kujaribu kuhamia Ulaya, ambazo hazikufanikiwa.
Mshambuliaji wake mwingine, Mzambia Felix Sunzu ambaye kwa wiki nzima yuko kwao kwenye msiba wa dada yake, alirejea jana na jioni alifanya mazoezi, tayari kwa mechi ya leo.
Lakini Simba pia inajivunia mshambuliaji wake kutoka Ghana, Daniel Akuffo ambaye hadi sasa katika mechi nne za kirafiki, amefunga mabao matatu, ingawa hiyo ambayo hakufunga, dhidi ya Sofapaka hakumaliza hata nusu ya kwanza ya mchezo, baada ya kuumia na kutoka.
Viungo Mrisho Khalfan Ngassa na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ kwa mara ya kwanza leo watacheza dhidi ya timu yao ya zamani- wote hawa waliichezea Azam ilipoifunga Simba 3-1 katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame Julai 24, mwaka huu Uwanja wa Taifa.
Azam itakayotokea Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi zake zote nne za kujipima nguvu, dhidi ya Prisons 1-0, Transit Camp 8-0, Coastal Union 2-0 na Azam Akademi 4-0.
John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote matatu Simba ilipokutana na Azam mara ya mwisho na mwenye kawaida ya kufunga kila mechi baina ya timu hizo, leo kwa mara nyingine atakuwa tishio kubwa kwa Wekundu wa Msimbazi, akicheza mbele ya kiungo bora kwa sasa Afrika Mashariki, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’.
Beki wa zamani wa Simba SC, Mganda Joseph Owino bado hajamshawishi kocha mpya wa Azam, Boris Bunjak na hapana shaka leo Said Mourad atacheza pamoja na Aggrey Morris katika beki ya kati, juu yao akisimama Jabir Aziz na Abdi Kassim ‘Babbi’ anaweza kuanza na Adebayor pale mbele.
Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.
Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu, Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na kiraka Shomari Kapombe. 


Vikosi vya leo;
Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyosso, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Daniel Akuffo na Emanuel Okwi.
Azam FC; Deo Munishi ‘Dida’, Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad, Aggrey Morris, Jabir Aziz, Kipre Michael Balhou, Salum Abubakar, John Bocco, Abdi Kassim na Kipre Herman Tchetche.

REKODI YA SIMBA NA AZAM
Julai 24, 2012
Simba 1-3 Azam (Robo Fainali Kagame)
Julai 12, 2012
Simba 2-2 Azam (Fainali Urafiki Cup)
(Simba ilishinda kwa penalti 3-1)
Februari 11, 2012
Simba SC 2 - 0 Azam FC
Sept 11, 2011

No comments:

Post a Comment