Thursday, December 29, 2011

Tasnia ya muziki yapata pigo kubwa: andy brown swebe 'Ambassador' hatunaye tena


Mwanamuziki wa siku nyingi nchini ambaye aliondokea kuwa mahiri katika gitaa la bezi Andy Brown Swebe aka ambasador (pichani) amefariki dunia leo baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kwa mujibu wa mwanamuziki Kitime aliyefika katika ofisi za HabariLeo majira ya mchana, Swebe alifariki majira ya saa 10 alfajiri katika hospitali ya Marie Stoppes ya Mwenge alipokuwa amekimbizwa kwa ajili ya tatizo la pumu.

Mipango ya maziko ya Andy Brown Swebe ambaye alianza kupenda gitaa kutokana na kumsikia baba yake mzee Mwalimu Brown Samson Swebe akifanya vitu vyake, inafanyika nyumbani kwao Sinza Mori.

Kama Miezi miwili iliyopita mwanamuziki huyo alikuwa katika safari ya kikazi nchini Marekani ambako aliambatana na King Kiki na Maneno Uvuruge.Kitime alisema zaidi kwamba mipango ya maziko inasubiri baba zake wakubwa kutoka Tukuyu, Mbeya.
Swebe ambaye alianza kujifunza kupiga gitaa huko Chang’ombe kwa David Musa wa Safari Trippers,bendi yake ya kwanza ilikuwa ni ya Oshekas ya Brian Shaka ambapo ilikuwa inapiga mara moja kwa mwezi Yatch Club.

kwa mujibu wa mkongwe John  Kitime, alipiga bendi hii mpaka alipomaliza kidato cha nne, ndipo alipopata kazi na kuhamia Morogoro, huko akawa anafanya kazi kiwanda cha ngozi.

Siku moja Orchestra Makassy ilifanya ziara Morogoro, na hapo rafiki yake aliyekuwa anapiga Keyboards katika bendi hiyo John Bosco akamuona na akakaribishwa jukwaani na akapiga nyimbo chache jambo ambalo lilifanya Mzee Makassy amwite katika bendi yake.

Alijiunga na Makassy Mei 25,1983 na onyesho la kwanza lilikuwa Mkirikiti Bar Msasani. Akiwa Orchestra Makassy alishiriki kurekodi nyimbo kama Olenge, Bembeya, Nono, Minachoka ya Masiya Radi. Wakati huo bendi ilikuwa na wakongwe kama Mzee Aimala Mbutu(Simaro), Fan Fan Mosesengo, Kassim Mganga na Dk Remmy.

Mwezi uliopita hayati Andy Swebe alikuwa Marekani na King Kikii na Maneno Uvuruge kuburudisha wakati wa sherehe za Miaka 50 ya Uhuru huko jijini Washington DC na vitongoji vingine vya Marekani. 

No comments:

Post a Comment