Ndugu wana Habari, najua kwamba
taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga wanaotuunga mkono,hasa
ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati ya utendaji vilivyopita
kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma ya mkutano mkuu ambao
tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo la kujiuzulu
linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa wajumbe wa
kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru wajumbe kwamba tulifanya
kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale tulipotofautiana
tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote tulikuwa tunawajibika
nayo.
Tangu tumeingia madarakani tumeweza
kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha mwaka mmoja, yaani;
Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011, na Ubingwa
wa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa
uteja kwa watani wetu wa jadi kila tulipokutana katika ligi ukiachia mbali
mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku
mkubwa katika klab yetu.Hali kadhalika tumeshirikiana mpaka tumeweza
kuboresha mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia
mkataba na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa
mafia na uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati
miliki za maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za
mwisho za kumalizia michoro.Hali kadhalika tuliingia mkataba wa kuzalisha na
kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada ya kufanya marekebisho yatokanayo
na matakwa ya sheria kule BRELA na pia mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo
itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje na ndani, kufanya promosheni zetu na
kampeni kwa njia ya electronic kupitia mitandao mbalimbali na kukusanya data za
wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi
300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu.
Haya yote tuliyafanya tukilenga
kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu
mmoja mmoja.Kwa ridhaa yenu tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni
mbali mbali kwa ajili ya udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati
ya makabidhiano kwa kiongozi ajaye.Aidha, tumeshirikiana katika kufanya mambo
mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya
Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na waliokumbwa na maafa, na kongamano
la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua nafasi yao katika Yanga ikiwa
ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS ya Yanga, ambapo maombi yapo
kwa msajili Manispaa ya Ilala.Haya yote nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa
ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha yaliyobaki ambayo mtaona
yalikuwa mazuri.Lakini pia tulipopata matatizo tulikuwa pamoja.
Nichelee kusema tu kwamba tulisimama
pamoja baada ya kujiuzulu Makamu Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe
wetu ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo, kwani tulifungwa na
katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu ndugu Yusuf M. Manji,
aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa ameonyesha nia ya kurudi
nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia kila jitihada za kumrejesha
lakini ikashindikana.Hata hivyo doa limetupata baada ya kufungwa na watani wetu
goli 5 bila, ambapo kuna wanachama wanaoelewa na wasioelewa kabisa.Ninachokiona
mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na
yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia.
SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa mfululizo wa matukio wiki
tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa
ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema.Sioni mantiki katika hoja kwamba
wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu
alishikiliwa Arusha kwa deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!Kwa wanaoijua
Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa
ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi
kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado
wachezaji walicheza kwa morali.Hata hivyo, utamaduni wa kutimuana baada ya
matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama hatutaiacha, kwani wenye hila na
uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo ili kuuondoa uongozi wa
kidemokrasia.
Baada ya mapinduzi kushindikana na TFF
kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia msemaji wao , Mzee Akilimali
wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini
wakidai kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea
kuongoza!Hii imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa
wanawake wawili waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa
nusu. Yule mwenye mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata
nusu.Kwa hekma hiyo nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa
Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya
28 ya katiba yetu.Vile vile siko tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au
kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni kiongozi.
Natumaini kamati ya utendaji kwa pamoja
na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya Yanga pamoja na bodi
ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano mkuu kwa
mafanikio zaidi. Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na nitatoa mchango
wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo wa
kufanya hivyo.
YANGA DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.
Nakala kwa:-Mama Fatma
Karume,MdhaminiFrancis Kifukwe, MdhaminiBwana Yusuf Manji – Kwa taarifa
No comments:
Post a Comment