FIDIA YA KIMBANGULILE KWA SAMATA
Kamati  ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa  Miguu Tanzania (TFF) chini ya uenyekiti wa Alex Mgongolwa ilikutana  Desemba 30 mwaka jana kupitia masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele  yake ikiwemo taarifa ya uamuzi wa timu ya Kimbangulile kukata rufani  Kamati ya Rufani kupinga uamuzi wake juu ya mchezaji Mbwana Samata.
Ikumbukwe  kuwa Kimbangulile iliwasilisha malalamiko TFF ikieleza kuwa inastahili  malipo baada ya Simba kumuuza Samata kwa timu ya TP Mazembe ya Jamhuri  ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kimbangulile  ilitaka ilipwe fidia ya mazoezi (training compensation) na mchango  maalumu (solidarity contribution) kwa mujibu wa Kanuni za Uhamisho wa  Wachezaji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Uamuzi  wa Kamati ya Mgongolwa ulikuwa Kimbangulile imeshindwa kutoa vielelezo  kuonesha kuwa iliingia gharama za mazoezi kwa mchezaji husika wakati  akiichezea timu hiyo.
Kwa upande wa  solidarity contribution ambayo ni asilimia 5 ya mauzo ya mchezaji huyo  TP Mazembe, fedha hizo zinatakiwa kulipwa na klabu yake hiyo mpya ambayo  TFF itaitaka kufanya hivyo wakati Samata atakapoombewa Hati ya Uhamisho  wa Kimataifa (ITC). Hivyo Kamati itatengeneza utetezi wake na  kuuwasilisha kwenye Kamati ya Rufani itakaposikiliza rufani ya  Kimbangulile.
USAJILI WA DIRISHA DOGO 2011/2012
Kwa  upande wa Daraja la Kwanza, Kamati hiyo imetoa siku saba kwa klabu  ambazo zimezidisha idadi ya wachezaji ili zipunguze, kwani kila timu  inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 30.
Klabu  nyingi baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo zimepitisha idadi ya  wachezaji 30 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni. Hivyo kwa klabu ambayo  itashindwa kupunguza wachezaji ndani ya muda huo, TFF itahesabu hadi 30  na wachezaji watakaokuwa wamezidi wataondolewa.
Kwa  klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), klabu ya Villa Squad ndiyo imekutwa  na kasoro katika usajili wake ambapo imetoa kwa mkopo wachezaji wanne  na imepokea wengine watano kwa mkopo.
Kwa  mujibu wa kanuni ya mkopo, klabu haitakiwi kuwa na wachezaji zaidi ya  watano iliotoa au kuingiza kwa mkopo kwa wakati mmoja. Hivyo Villa Squad  imetakiwa kuwaandikia barua za kuwaacha wachezaji wanne iliowatoa kwa  mkopo ili wawe huru (free agents).
Pia  Kamati imeagiza viongozi wa juu wa Majeshi ambayo yanamiliki timu za  mpira wa miguu kupewa elimu ya kanuni za usajili, kwani mafunzo ya  kijeshi na uhamisho wa wachezaji ambao ni askari vimekuwa vikiathiri  viwango vya timu zao kwenye ligi.
SIMBA KUMSIMAMISHA KOCHA BASENA
Malalamiko  ya Kocha Moses Basena kwa TFF baada ya klabu yake ya Simba kusimamisha  mkataba wake yaliwasilishwa mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi  za Wachezaji.
Baada ya kupitia  malalamiko hayo, uamuzi wa kamati ni kuwa suala hilo liendelee kuwa kati  ya Simba na Basena na kuwataka wakae pamoja ili waweze kulipatia  ufumbuzi.
Licha ya Basena kuwa na  mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, Kamati imebaini kuwa hauwezi  kufanya kazi (functional) kwa vile kocha huyo hakuwa na kibali cha  kufanya kazi nchini (work permit).
Hivyo  kisheria hakukuwa na mkataba kwa vile ili Basena aweze kuitumikia Simba  ni lazima awe na kibali cha kufanya kazi nchini. TFF ilikataa maombi ya  Simba kuiandikia barua Idara ya Uhamiaji kuthibitisha barua ya  kumuombea work permit baada ya kocha huyo kushindwa kuwasilisha vyeti  vyake vya ukocha.
Kwa vile Simba  imeshaajiri kocha mwingine (Milovan) kwa mkataba wa miezi sita na  kupatiwa kibali cha kufanya kazi nchini, ufumbuzi wa suala la Basena  unabaki kuwa kati ya klabu hiyo na kocha huyo.

No comments:
Post a Comment